Mar 21, 2019 04:41 UTC
  • Utawala wa Kizayuni wa Israel; nembo ya wazi ya jinai dhidi ya binadamu

Kamati ya Kutafuta Ukweli ya Umoja wa Mataifa imetoa ripoti kuhusiana na maandamano yaliyoanza mwaka 2018 katika mpaka wa Gaza, uvamizi na ukandamizaji wa Israel na kutoa orodha ya Wazayuni ambao imewatuhumu kwa kutenda jinai hatari katika matukio hayo.

Ripoti hiyo inatarajiwa kuwasilishwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Ripoti hiyo imeitaja Israel kwamba, ilikiuka haki za binadamu katika ukandamizaji uliofanywa na wanajeshi wa utawala huo dhidi ya waandamanaji wa Kipalestina kwenye Ukanda wa Gaza mwaka jana na ukandamizaji huo unaweza kuhesabiwa kuwa ni jinai ya kivita.

Ripoti ya Kamisheni Huru ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa yenye kurasa 250 na iliyotolewa siku ya Jumatatu  inaeleza kuwa, wanajeshi wa Israel wamekanyaga haki za kimataifa za binadamu kutokana na kutumia risasi hai dhidi ya waandamanaji wa Palestina wasio na silaha na kwamba, hiyo ni jinai dhidi ya binadamu. Kwa mujibu wa vigezo vya sheria, kuwauwa kwa makusudi raia ambao hawakushiriki moja kwa moja katika vitendo vya hasama na uadui, kunahesabiwa kuwa ni jinai ya kivita. 

Santiago Canton, Mkuu wa Kamisheni Huru ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Gaza

Hali ya wasiwasi ilizuka katika Ukanda wa Gaza tarehe 30 Machi 2018, baada ya wananchi wa Palestina kuanzisha mlolongo wa maandamano ya "Haki ya Kurejea" katika mpaka wa Gaza na ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.

Hadi sasa Wapalestina zaidi ya 270 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 27,000 wamejeruhiwa katika maandamano hayo. Aidha walenga shabaha wa Israel wamekuwa wakiwafyatulia risasi  kwa makusudi watoto, wafanyakazi wa mashirika ya misaada na waandishi wa habari.

Hivi karibuni Santiago Canton, Mkuu wa Kamisheni Huru ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Gaza alitangaza katika ripoti yake kwamba: Wanajeshi wa Israel wamekiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu na haki za kiutu. Canton amesisitiza kuwa, uhalifu huo ni jinai za kivita au jinai dhidi ya binadamu.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza mara chungu nzima kwamba, Israel ilitenda jinai wakati wa kukabiliana na maandamano ya Wapalestina ya "Haki ya Kurejea" huko Gaza.

Mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza

Maandamano ya amani ya Wapalestina ya "Haki ya Kurejea" yaliyoanza Machi mwaka jana katika Ukanda wa Gaza yangali yanaendelea huku wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel wakishadidisha ukandamizaji na mauaji yao dhidi ya Wapalestina siku baada ya siku.

Kwa hakika jinai dhidi ya binadamu ni miongoni mwa jinai ambazo zilianza kutelezwa na Israel hata kabla ya kuasisiwa utawala huo bandia Mei 14 mwaka 1948. Jinai hizo zimekuwa zikifanywa na Israel kwa sura tofauti kama mauaji, kuwafanya kuwa wakimbizi Wapalestina, kuwabaidisha na kuwaua wananchi madhulumu wa Palestina.

Hapana shaka kuwa, kile ambacho kinafanyika huko Gaza zikiwemo hatua za kuzuia kuingizwa katika eneo hilo bidhaa za chakula, dawa na kutoruhisiwa kuondoka katika eneo hilo wagonjwa wenye hali mbaya kwa ajili ya kwenda kutibiwa sehemu nyingine na vilevile kuteswa mateka ni mifano ya wazi ya kuangamiza kizazi na jinai za kibaguzi mambo ambayo yametajwa katika kifungu cha saba cha hati ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwamba, ni katika ya mambo yanayohesabiwa kuwa ni jinai dhidi ya binadamu.

Wanajeshi wa utawala dhalimu wa Israel

Kile ambacho kiko wazi ni kwamba, hatua za Israel za kuwaua Wapalestina ni mfano wa wazi kabisa wa jinai dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari. Kushika kasi jinai za Israel katika miaka ya hivi karibuni hususan mashambulio yake ya kinyama huko Gaza nako kumezijeruhi na kuzitia simanzi mno nyoyo za walimwengu wenye dhamira safi.

Kwa hakika jinai za Israel ni kubwa na za kutisha kiasi kwamba, katika miezi ya hivi karibuni asasi na jumuiya mbalimbali za kimataifa za kutetea haki za binadamu zinazofungamana na Umoja wa Mataifa zimelifanya suala la kufanya uchunguzi katika uwanja huo kuwa miongoni mwa ajenda zake kuu. Hapana shaka kuwa, hatua hizi za Israel zinazidi kudhihirisha utambulisho halisi wa utawala huo ghasibu ulio dhidi ya ubinadamu na kuufanya utambuliwe na walimwengu kuwa nembo ya jinai dhidi ya binadamu.

Tags

Maoni