Mar 25, 2019 00:15 UTC

Adil al Kalbani, imam wa zamani wa Msikiti wa Makka (Masjudul Haram) amebadilisha msimamo wake kuhusiana na Waislamu wa Kishia.

Akihojiwa na kanali ya televisheni ya MBC ya Saudi Arabia, Kalbani amesema kuwa yeyote anayetamka Laailaah Illa Llah (لا اله الا الله) na kufuata Kibla chetu huyo si kafiri.

Amma kuhusiana na uwalii wa mwanamme kwa mwanamke, imam huyo wa zamani wa Msikiti wa Makka amesema kuwa, sasa inaruhusiwa mwanake kwenda nchini Marekani bila ya kufuatana na mahramu wake kwani muda wa safari kutoka Saudi Arabia hadi Marekani ni masaa 12 yaani chini ya usiku na mchana.

Wanawake wa Saudia wakishangiria muziki wa POP uliopigwa kwa mara ya kwanza na mwanamuziki Tamer Hosny (raia wa Misri) nchini Saudi Arabia mwezi Aprili 2018

 

Hata hivyo amesema si sahihi kuondoa kikamilifu uwalii wa mwanamme kwa mwanamke kwani ndoa yoyote haiwezi kusihi bila ya kuwepo walii na mashahidi wawili waadilifu. Ikumbukwe kuwa, huko nyuma al Kalbani alikuwa anaharamisha jambo lolote linalokwenda kinyume na mila na desturi za Saudia.

Hata hivyo, hivi sasa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, Muhammad bin Salman amezusha wimbi jipya ambalo limeruhusu kupigwa miziki waziwazi katika majumba ya starehe, vinanda na kuhudhuria wanawake na wanaume kwenye sherehe, suala ambalo limepelekea masheikh wa serikali nao wabadilishe mno misimamo yao.

Alipoulizwa ni kwa nini amebadilisha msimamo, Kalbani amesema, kwani kuna tatizo lolote kwa mtu kusema kitu halafu akabadilisha msimamo wake? Kwanza nilikuwa nikiamini kuwa muziki ni haramu, lakini sasa mtazamo wangu umebadilika, kuna tatizo lolote hapo?

Aidha amekosoa fikra iliyoenea Saudi Arabia ya kutokubali mawazo ya wengine akisema kuwa, anatumai jamii ya Saudia itaendelea na kupiga hatua itakayoifanya ikubaliane na mawazo ya watu wengine.

Maoni