Mar 25, 2019 07:33 UTC
  • Uungaji mkono wa mirengo yote ya Lebanon kwa Hizbullah na kudhalilika kwa Pompeo

Siku ya Ijumaa, Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, aliwasili mji mkuu wa Lebanon, Beirut kwa madhumuni ya kwenda kutafuta uungaji mkono wa shakhsia na makundi ya kisiasa ya nchi hiyo dhidi ya Hizbullah, lakini alikabiliwa na jibu moja la Walebanon la kuiunga mkono harakati hiyo ya muqawama.

Katika kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita, serikali ya Marekani inayoongozwa na Donald Trump imeonyesha kuwa haisiti kuchukua hatua yoyote ile kwa uwazi na bila kificho ya kuiunga mkono Israel, ambapo kuhusiana na suala hilo tunaweza kuashiria maamuzi kadhaa yaliyo kinyume cha sheria iliyochukua, ikiwemo kuitangaza Quds tukufu kuwa mji mkuu wa Israel, kuuhamishia katika mji huo ubalozi wa Marekani uliokuweko Tel Aviv na vile vile kuyatambua rasmi mamlaka na umiliki wa Israel kwa eneo la miinuko ya Golan ya Syria unalolikalia kwa mabavu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo

Lakini mbali na hayo, serikali ya Trump imechukua hatua nyingine pia kwa ajili ya kuuhami utawala wa Kizayuni wa Israel ikiwemo kuitangaza Hizbullah ya Lebanon kuwa ni kundi la kigaidi na kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo kwa lengo la kuisukuma harakati hiyo ya muqawama nje ya ulingo wa siasa za nchi hiyo. Katika safari ya karibuni iliyofanywa na Mike Pompeo nchini Lebanon, ambayo ni ya kwanza nchini humo tangu alipoteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, njama hiyo chafu ya Washington imefuatiliwa tena na bila ya kificho. Gazeti la Al-Diyar linalochapishwa nchini Lebanon, limeizungumzia safari ya Pompeo kwa kuandika: "Safari ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani haikuwa na ujumbe wowote mpya kwa Walebanon, kwani viongozi wa Lebanon walisikia maneno yale yale ya kukaririwa ya huko nyuma, ambayo yanabeba ajenda mbili za msingi, nazo ni: Kuzidisha mashinikizo dhidi ya Hizbullah na kukabliana na Iran nchini Lebanon."

Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah

Hata hivyo makundi na mirengo ya kisiasa ya Lebanon imeonyesha msimamo wa wazi katika kukabiliana na harakati na chokochoko za waziri wa mambo ya nje wa Marekani dhidi ya Hizbullah. Sababu kuu ya kushuhudiwa msimamo mmoja na mtazamo wa umoja kati ya makundi yote ya Lebanon kuhusiana na Hizbullah, ni nafasi ya kisiasa na ya uungaji mkono wa umma iliyonayo harakati hiyo nchini humo. Njama za Marekani dhidi ya Hizbullah zinafanywa katika hali ambayo, muungano wa muqawama ulioongozwa na harakati hiyo ulinyakua jumla ya viti 68 katika uchaguzi wa bunge uliofanyika Mei 2018, na hivyo kupata zaidi ya viti 64 jumlisha na kimoja. Kwa maneno mengine ni kwamba, muungano wa muqawama ulipata wingi mutlaki wa viti katika uchaguzi huo uliopita wa bunge la Lebanon. Ushindi huo ni kielelezo cha wazi cha nafasi ya Hizbullah na kukubalika kwake mbele ya umma wa Walebanon waliowengi, nukta ambayo hata Rais Michel Aoun wa nchi hiyo aliiashiria pia katika mazungumzo yake na Pompeo. Kiongozi huyo alimueleza waziri wa mambo ya nje wa Marekani kwamba: "Hizbullah imetokana na msukumo wa wananchi na inashiriki katika bunge na serikali ya Lebanon. Lakini zaidi ya hayo, Hizbullah inawakilisha moja ya madhehebu kuu za dini ndani ya ardhi na nchi yake."

Rais Michel Aoun (kulia) katika mazungumzo na Pompeo

Harakati ya Hizbullah inashikilia pia nafasi kadhaa za uwaziri katika serikali ya Lebanon; na hata ikilinganishwa na serikali iliyopita ya Waziri Mkuu Saad Hariri, nafasi ya harakati hiyo katika serikali mpya ya Hariri ni kubwa zaidi. Ni kama alivyoeleza Hassan Qablan, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Amal kwamba, Saad Hariri  anatambua vyema mlingano wa nguvu za kisiasa ndani ya Lebanon, ambayo ndiyo sababu ya kuwepo uthabiti nchini humo. Na ndiyo maana wakati Pompeo alipozungumzia suala la kutoa mashinikizo kwa Hizbullah katika mkutano wake na Hariri, waziri mkuu huyo wa Lebanon alimsisitizia waziri huyo wa serikali ya Trump kwa kumwambia: "Lebanon haitaki kujiingiza kwenye mizozo ya siasa na sera za nje za Marekani."

Kwa kuzingatia hali hiyo, tuna kila sababu ya kusema kuwa, waziri wa mambo ya nje ya Marekani hakuambulia chochote katika safari aliyofanya nchini Lebanon; na kitu pekee alichosikia kutoka kwenye vinywa vya viongozi wa nchi hiyo, ni uungaji mkono wao wa pande zote kwa harakati ya muqawama ya Hizbullah.../

Tags

Maoni