Mar 25, 2019 07:59 UTC
  • Hizbullah: Hatutorudi nyuma katika kuwalinda raia wa Lebanon kutokana na hujuma za Israel

Naibu Mkuu wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon amesisitiza kwamba muqawama huo hautoachana na majukumu ya kuwalinda raia wa Lebanon kutokana na hujuma za utawala katili wa Israel.

Sheikh Ali Da'mush ameongeza kwamba, muqawama wa Hizbullah utaendeleza njia yake, licha ya kuwepo njama tofauti za Marekani na utawala haramu wa Kizayuni. Ameongeza kwamba katika miaka kadhaa iliyopita, ikiwemo 1993, 1996 na 2006 Marekani na Israel zimetumia kiasi kikubwa cha mamilioni ya Dola kwa ajili ya kuisambaratisha au kuidhoofisha harakati ya Hizbullah, njama ambazo hata hivyo zimeishia kufeli.

Sheikh Ali Da'mush, Naibu Mkuu wa Baraza la Utekelezaji wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon

Kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon amesema kuwa katika uchaguzi wa bunge wa mwaka jana nchini humo, Marekani na Israel sambamba na kueneza urongo, vitisho na uchochezi zilifanya njama kubwa pia za kuwazuia wananchi kuipigia kura harakati hiyo, hata hivyo msimamo na mshikamano wa Walebanon vilifanikiwa kusambaratisha njama hizo kwa kuwapigia kura wawakilishi wa Hizbullah bungeni. Katika safari yake ya siku mbili za tarehe 22 na 23 za mwezi huu nchini Lebanon, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alifanya juhudi nyingi kwa ajili ya kuyachochea makundi ya kisiasa ya nchi hiyo dhidi ya Harakati ya Hizbullah kwa lengo la kuibua tofauti kati yao, hata hivyo alikabiliwa na jibu kali na la wazi kutoka kwa viongozi wa Lebanon waliomwambia kwamba harakati hiyo ni sehemu ya serikali na bunge la nchi hiyo.

Tags

Maoni