Mar 26, 2019 07:28 UTC
  • Vita vya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen vyaingia mwaka wa tano

Vita vya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen ambavyo vilianza tarehe 26 Machi mwaka 2015, leo vinaingia mwaka wake wa tano.

Wakati Saudia ilipoanzisha hujuma dhidi ya nchi hiyo masikini zaidi ya Kiarabu katika eneo la Asia Magharibi, ilikuwa imetathmini kuwa vita hivyo havitaendelea kwa zaidi ya wiki tatu. Lengo kuu la Saudia katika kuanzisha vita hivyo lilikuwa ni kuiondoa harakati ya Ansarullah madarakani na kuifanya irejee katika hali ya kutengwa kama ilivyokuwa kabla ya mwezi Septemba mwaka 2014. Hivi sasa miaka minne baada ya vita hivyo haramu, si tu kuwa Ansarullah haijarejea katika hali ya kabla ya Septemba 2014, bali hivi sasa Ansarullah ni mhimili mkuu wa nguvu na utawala nchini Yemen na hakuna mazungumzo yanayoweza kufanyika Yemen pasina kuishirikisha harakati hiyo.

Mbali na hayo, ukoo wa Aal Saud unaotawala Saudia, baada ya kuanzisha vita dhidi ya Yemen ulitangaza kuwa lengo la vita hivyo ni kurejesha kile ulichodai kuwa ni "uhalali" na hapo kusudio lilikuwa ni kumrejesha madarakani kibaraka wake aliyejuzulu kama rais wa Yemen na kutoroka nchi, Abdu Rabbuh Mansour Hadi.

Hivi sasa baada ya kumalizika mwaka wa nne wa vita vya Saudia dhidi ya Yemen, Mansour Hadi bado yuko Riyadh na si tu kuwa hajaweza kurejea Sanaa bali kwa mtazamo wa Wayemen waliowengi, amefanya uhaini mkubwa kwa kuunga mkono vita vya Saudia ambavyo vimesababisha umwagaji damu ya wananchi wasio na hatia.

Abdu Rabuh Mansour Hadi aliyekuwa rais wa Yemen ambaye ni kibaraka wa Saudia na Imarati ametajwa na Wayemen kuwa msaliti mkubwa

Saudi Arabia na waitifaki wake katika vita vya Yemen wametenda jinai kwa mujibu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC. Jinai hizo ni pamoja na jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu, jinai dhidi ya amani na jinai ya uvamizi. Kuna nyaraka na ushahidi wa wazi kuhusu jinai hizo za Saudia na waitifaki wake dhidi ya watu wa Yemen.

Yusuf Al Hadhri, Msemaji wa Wizara ya Afya ya Yemen katika taarifa kuhusu vita vya Saudia dhidi ya Yemen amesema, katika kipindi cha miaka minne ya vita hivyo watu  12,000 wameuawa moja kwa moja vitani huku wengine 26,000 wakiwa wamejeruhiwa. Aidha amesema katika kipindi hicho, wagonjwa 32,000 Wayemen wameaga dunia kutokana na kuwa hawawezi kuenda nje ya nchi kupata matibabu kufuatia mzingiro uliowekwa na muungano huo vamizi wa Saudia. Kwa maneno mengine ni kuwa watu 44,000 wamefariki dunia nchini Yemen kutokana na vita kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Miongoni mwa waliofariki kuna wanawake na watoto 6,361.

Halikadhalika kati ya taathira zingine za vita vya Saudia dhidi ya Yemen ni kuenea magonjwa hatari na maambukizi nchini humo. Kwa mujibu wa takwimu, karibu Wayemen milioni moja na laki nne wanaugua kipindupindu na tayari watu 3,000 wameshafariki kutokana na ugonjwa huo.

Hali kadhalika vita hivyo vya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen vimepelekea karibu Wayemen milioni 3 kuwa wakimbizi na kati ya watu milioni 24 nchini Yemen, takribani milioni 22 wanahitaji msaada wa chakula. Aidha karibu watoto milioni 3 nchini Yemen wanakabiliwa na lishe duni ambapo laki nne miongoni mwao wanakabiliwa na hali mbaya sana na wanaweza kufariki dunia wakati wowote. Kwingineko vita vya Saudia dhidi ya Yemen vimepelekea asilimia 80 ya miundo msingi ya nchi hiyo kuteketea. Kwa ujumla ni kuwa hali hiyo imepelekea taasisi za kimataifa kutangaza kuwa maafa ya kibinadamu Yemen ni mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miongo ya hivi karibuni.

Pamoja na hayo yote, katika kuanza mwaka wake wa tano, vita hivyo vinaelekea wapi?

Inaelekea kuwa, vita vya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen vitaendelea kwa sababu kadhaa. Awali ni kuwa utawala wa Saudia haujafikia malengo yake katika vita hivyo na hivyo kumalizika vita kutakuwa na maana kuwa Saudia imekubali kushindwa. Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudia ambaye alianzisha vita dhidi ya Yemen alikuwa na dhana kuwa vita hivyo vitampelekea aonekane shujaa katika Ulimwengu wa Kiarabu na hivyo kukubali kushindwa si jambo lililo katika fikra ya mwanamfalme huyo aliyejawa na kiburi. Bin Salman yuko tayari kuona makumi ya maelfu ya Wayemen wengine wasio na hatia wakiuawa kwa ajili ya kiburi chake tu.

Watoto wa Yemen ni waathirika wakuu wa vita vya Saudia dhidi ya nchi yao

Nukta ya pili ni kuwa, mafanikio ya sasa ya kijeshi ya Harakati ya Ansarullah na Jeshi la Yemen hayawezi kulinganishwa na miaka minne iliyopita hasa kwa kuzingatia uwezo mkubwa wa kijeshi wa pande hizo mbili. Hivi sasa Jeshi la Yemen ambalo linashirikiana kwa karibu na wapiganaji wa Ansarullah limepata uwezo mkubwa wa kuipa Saudia pigo kubwa la kijeshi. Nukta ya tatu ni kuwa mapatano ya amani ya Stockholm ya Disemba mwaka 2018 ambayo yalisimamiwa na Umoja wa Mataifa yamefeli kutokana na uafriti na ukwamishaji wa Saudia.

Ukweli wa mambo ni kuwa, mgogoro wa Yemen utamalizika tu iwapo madola makubwa duniani, hasa Marekani, yatakuwa na irada ya kukabiliana na jinai za Saudia. Aidha vita hivyo vinaweza kumalizika iwapo jamii ya kimataifa itaushinikiza utawala vamizi wa Saudia. Lakini hivi sasa inaonekana kuwa Marekani , ambayo inaongoza katika kuiuzia Saudia silaha inazotumia dhidi ya watu wa Yemen, haiko tayari kuishinikiza Saudia bali hata utawala wa Trump uko tayari kuendelea kuunga mkono jinai za Saudi Arabia huko Yemen ili kuendelea kupata faida za kifedha zinazotokana na vita hivyo.

Maoni