Mar 26, 2019 07:32 UTC
  • Syria: Tangazo la Trump kuhusu Golan haliwezi kubadilisha chochote

Syria imesema hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani kutambua rasmi Miinuko ya Golan kuwa milki ya utawala haramu wa Israel katu haiwezi kubadilisha ukweli kwamba miinuko hiyo ni mali halali ya Syria.

Wallid al-Muallim, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema serikali ya Marekani haina mamlaka yoyote kuhusu miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Kizayuni na kwamba azimio lililosainiwa na Trump la kuitambua miinuko hiyo kuwa mali ya Israel halitakuwa na taathiri yoyote kuhusu eneo hilo.

Amesema, "Hatua hiyo ya Trump haitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuifanya Marekani itengwe. Alianza na Jerusalem (Quds), lakini hapa hawezi kufanya chochote kuhusu Golan, ardhi hiyo ni mali na milki ya taifa la Syria."

Trump jana Jumatatu alitekeleza vitisho vyake, kwa kusaini eti azimio la kuitambua Miinuko ya Golan ya Syria kuwa mali ya utawala wa Kizayuni wa Israel, hatua ambayo imeendelea kukosolewa katika kila kona ya dunia.

Wanazuoni na wananchi wa Syria katika milima ya Golan

Utawala wa Kizayuni wa Israel uliivamia na kuiteka milima ya Golan ya Syria mwaka 1967. Eneo hilo lenye ukubwa wa takriban kilomitamraba 200 ni miliki ya Syria isiyotenganishika na ardhi nyingine za nchi hiyo ya Kiarabu.

Ukiachilia mbali Marekani na utawala wa Kizayuni, jamii nzima ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zimetangaza rasmi kuwa milima ya Golan ni mali ya Syria.

Kadhalika azimio nambari 242 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ni miongoni mwa nyaraka muhimu za jamii ya kimataifa ambazo zilitupilia mbali madai ya Israel ya kutaka kujimilikisha miinuko hiyo ya Golan.

Tags

Maoni