Apr 22, 2019 14:54 UTC
  • Mamluki 54 wa Saudia waangamizwa katika shambulizi la kombora la Yemen

Msemaji wa vikosi vya ulinzi Yemen amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limeshambulia maeneo ya muungano vamizi wa Saudi Arabia kwa kombora la Badr-F na kuangamiza wavamizi 54.

Yahya Sarii amesema hayo leo na kuongeza kuwa shambulio hilo limefanyika katika eneo la Jizan lililoko katika mpaka wa Yemen na Saudi Arabia.

Televisheni ya al Masirah imemnukuu msemaji huyo wa majeshi ya Yemen akitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, 9 kati ya wavamizi hao 54 walioangamizwa kwenye shambulio hilo walikuwa ni maafisa wa kijeshi wa Saudi Arabia.

Ameongeza kuwa, makumi ya mamluki wa muungano vamizi wa nchi za Kiarabu unaoongozwa na Saudi Arabia wamejeruhiwa katika shambulizi hilo.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, shambulio hilo lilifanyika jana Jumapili katika eneo la magharibi mwa Jizan.

Mmoja wa mamluki wa Saudi Arabia aliyeuawa nchini Yemen

 

Msemaji huyo wa vikosi vya ulinzi vya Yemen ameongeza kuwa, shambulio hilo limefanywa kama sehemu ya kukumbuka mwaka wa kwanza tangu alipouawa shahidi Salih al Sammad, Rais wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen. 

Itakumbukwa kuwa tarehe 19 Aprili 2018, msafara wa al Sammad ulishambuliwa na ndege za kivita za muungano vamizi wa Saudia na kupelekea kuuawa shahidi mwanamapambano huyo na wenzake sita aliokuwa amefuatana nao. 

Kombora la Badr-F lina uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 160, na mripouko wake unaweza' kuathiri eneo lenye ukubwa wa mita 350. Limetengenezwa kwa zaidi ya vipande 14 elfu na uwezekano wa kukosea shabaha iliyolengwa na kombora hilo ni mita tatu tu.

Maoni