Apr 23, 2019 09:50 UTC
  • Usalama warejea Syria, wafanyaziara wa Iraq waingia kwa mabasi baada ya miaka 5 ya vita

Vyombo vya habari nchini Iraq vimeripoti kwamba kwa mara ya kwanza mabasi yaliyowabeba wafanyaziara wa Iraq yameingia Syria kwa ajili ya kufanya ziara katika maeneo matakatifu ya kidini ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mabasi mawili yaliyowabeba wafanya ziara wa Iraq yamewasili Syria kwa njia ya nchi kavu kwa ajili ya kuzuru haram ya Bibi Zainab (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) pamoja na maeneo mengine matukufu ya nchi hiyo. Habari zinasema kuwa mabasi hayo yameingia Syria kupitia kivuko cha al-Qaim kilichopo katika mipaka ya nchi mbili. Kivuko hicho kilidhibitiwa na magaidi wakufurishaji wa Daesh (ISIS) mwaka 2014 baada ya kundi hilo kudhibiti maeneo kadhaa ya nchi hiyo.

Haram ya Bibi Zaynab SA, mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW  nchini Syria

 

Mipaka ya pamoja ya Iraq na Syria yalikuwa chini ya udhibiti wa genge hilo kwa miaka kadhaa huku magaidi hao wanaoungwa mkono na Marekani, Israel, Saudia, Imarati na baadhi ya nchi za Kiarabu na Magharibi, wakifanya mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya Syria na Iraq. Hata hivyo majeshi ya Syria na Iraq kwa kushirikiana na washauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pia kwa uungaji mkono wa Russia, yameweza kuwafurusha magaidi hao na kuwaondoa katika maeneo hayo muhimu.

Hivi karibuni serikali ya Iraq ilitangaza habari ya kufikiwa makubaliano na serikali ya Syria kwa ajili ya kufunguliwa vivuko vya pamoja vya mpakani. Kivuko cha Abu Kamal katika jimbo la Deir ez-Zor nchini Syria pamoja na kivuko cha Qaim cha mkoa wa Al-Anbar nchini Iraq, ni vivuko ambavyo serikali hizo zilifikia makubaliano ya kuviweka wazi.

Tags

Maoni