Apr 24, 2019 07:57 UTC
  • Amnesty International: Saudia haiheshimu thamani ya utu

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limekosoa vikali kitendo cha utawala wa Aal-Saud cha kutekeleza hukumu ya kuwanyonga makumi ya Waislamu wa Kishia nchini Saudi Arabia, likisisitiza kuwa utawala huo wa kifalme hauheshimu thamani ya utu.

Mkurugenzi wa Utafiti wa shirika hilo katika eneo la Asia Magharibi, Lynn Maalouf amelaani vikali hatua ya watawala wa Riyadh kutumia kisingizio cha kupambana na ugaidi kuwanyonga kwa umati Waislamu wa Kishia.

Amnesty International imesema ni jambo la kusitikisha namna Riyadh inavyotumia 'Sheria ya Kupambana na Ugaidi' kuwabinya na kuwakandamiza Waislamu hao ambao ni katika jamii ya walio wachache nchini humo.

Mkurugenzi wa Utafiti wa shirika hilo amesema kiwango cha watu kuhukumiwa kifo nchini Saudi Arabia kinatia wasiwasi mkubwa na kwamba Riyadh inatumia hukumu hizo kukandamiza wapinzani na wakosoaji wake, kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kuimarisha usalama wa taifa.

Saudia ikitekeleza ukatili dhidi ya wanaharakati wa kisiasa

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limesema kitendo hicho cha kunyongwa makumi ya Waislamu wa madhrehebu ya Shia kilitekelezwa jana Jumanne, baada ya kukamilika mchakato bandia wa kesi dhidi ya watuhumiwa.

Jana Jumanne, watawala wa Aal-Saud waliwanyonga kwa kuwakata vichwa watu 37, aghalabu yao wakiwa Waislamu wa madhehebu ya Shia na kisha kuanika mwili wa mmoja wa Waislamu hao waliowafanyia ukatili huo kwenye kigingi hadharani kwa ajili ya kutazamwa na umati.

Maoni