• Indhari ya Ujerumani na Russia kuhusu hatari ya kutokea vita kati ya Marekani na Korea Kaskazini

Kuongezeka mivutano na kutoleana kauli za vitisho viongozi wa Marekani na Korea Kaskazini kumeitia wasiwasi mkubwa jamii ya kimataifa juu ya uwezekano wa kutokea vita katika eneo la Mashariki mwa Asia.

Kwa sababu hiyo, viongozi wa ngazi za juu wa nchi mbili muhimu za Ulaya na Eurasia yaani Ujerumani na Russia wametoa indhari juu ya suala hilo.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesisitiza kuwa hakuna njia yoyote ya utumizi wa nguvu za kijeshi itakayoweza kuhitimisha mzozo kati ya Marekani na Korea Kaskazini na kwamba vita vya maneno vinavyoendelea baina ya nchi hizo mbili si muelekeo sahihi wa kufuatwa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov, yeye amesema, uwezekano wa kutokea mapigano ya kijeshi kati ya Marekani na Korea Kaskazini umezidi kuwa mkubwa kutokana na vitisho vya waziwazi vinavyotolewa na Washington na Pyongyang vya kutumia nguvu za kijeshi. Dmitry Kurnif, mkuu wa kituo cha taaluma za kijeshi cha Russia anasema: "Korea Kaskazini iko tayari kuonyesha upinzani mkali wa kukabiliana na shambulio la aina yoyote". 

Rais wa Marekani na Kiongozi wa Korea Kaskazini

Licha ya kuwepo hitilafu na tofauti kati ya Ujerumani na Russia kuhusiana na mgogoro wa Ukraine, lakini inavyoonekana nchi hizo mbili kubwa za Ulaya na Eurasia zina mtazamo unaofanana kuhusu hali hatari iliyopo hivi sasa Mshariki mwa Asia na uwezekano wa kuzuka vita vikubwa katika eneo hilo la kistratijia. Kwa mujibu wa Constantin Asmaluf, mtaalamu wa masuala ya Korea, hata katika enzi za Vita Baridi hali ya mambo haikuwahi kuwa ya hatari katika Peninsula ya Korea kama inavyoshuhudiwa hivi sasa ya kuweza kusababisha kutokea Vita vya Tatu vya Dunia.

Japokuwa kila moja kati ya Ujerumani na Russia inataka zichukuliwe hatua za kuzuia kuendelea mgogoro uliopo kati ya Marekani na Korea Kaskazini kwa kuzingatia maslahi yake na kwa mtazamo tofauti na wa mwenzake, lakini zote mbili zinapigania kupatikana hatima moja juu ya kadhia hiyo. Ujerumani, ambayo ni nchi kubwa zaidi kiuchumi katika Umoja wa Ulaya inayofuata sera za usafirishaji bidhaa nje inalipa umuhimu mkubwa suala la kupanua zaidi wigo wa miamala yake ya kiuchumi na kibiashara na kustawisha uwekezaji wake katika nchi muhimu za Mashariki mwa Asia hususan China, Japan na Korea Kusini na vilevile nchi zinazojulikana kama Chui wa Asia. Kwa hivyo kuendelea mivutano ya kijeshi na kiusalama kati ya Marekani na Korea Kaskazini itakayovuruga uthabiti na kuzusha machafuko katika eneo hilo hasasi kutahatarisha usalama wake wa kiuchumi; na hilo litakuwa na madhara kwa Umoja wa Ulaya na Ujerumani.

Mfumo wa makombora ya kutungulia ndege THAAD uliowekwa Korea Kusini

Amma kwa upande wa Russia, kwa mtazamo wa viongozi wa nchi hiyo, kuendelea kuwepo kijeshi Marekani katika eneo la Mashariki mwa Asia na hatua kadhaa inazochukua ikiwemo ya kuweka mfumo wa kutungulia makombora THAAD ndani ya ardhi ya Korea Kusini, mbali na manuva makubwa na ya mtawalia ya kijeshi inayofanya kwa kushirikiana na Korea Kusini na Japan pamoja na kuzidi kuongezwa idadi ya askari wa Marekani katika eneo la Asia na Bahari ya Pasifiki, yote hayo ni tishio kubwa la kiusalama linaloilenga Russia na muitifaki wake yaani China. 

Katika kujibu mapigo ya kukabiliana na hatua hizo, Moscow na Beijing zimechukua hatua kadhaa ikiwemo kutangaza hadharani upinzani wao dhidi ya sera na hatua za Marekani, kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na kuzidisha harakati za ushirikiano wao wa kijeshi na kiusalama.

Wakati huohuo, msimamo wa pamoja na unaofanana ulioonyeshwa na Ujerumani na Russia kuhusiana na siasa za kushupalia vita za Rais wa Marekani Donald Trump na sisitizo lao juu la ulazima wa mgogoro huo kushughulikiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yote hayo yanaonyesha kuwa kuna aina fulani ya muungano usio wa maafikiano ya kimaandishi unaoanza kuundwa taratibu na madola makubwa kimataifa ya Magahribi na Mashariki dhidi ya sera za Trump. Misimamo iliyochukuliwa na kiongozi huyo katika masuala kadhaa kama upinzani wake dhidi ya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi, upinzani dhidi ya biashara huru pamoja na hatua za kihasama alizochukua dhidi ya Russia kwa kusaini sheria ya vikwazo vipya dhidi ya nchi hiyo, vimeufanya ulimwengu uanzishe upinzani dhidi ya Trump, mfano wa karibuni kabisa ukiwa ni huu ulioonyeshwa na Ujerumani na Russia wa kukosoa mielekeo ya kushupalia vita ya Rais wa Marekani dhidi ya Korea Kaskazini.../  

Aug 12, 2017 13:32 UTC
Maoni