• Uhalalishaji usio wa kimantiki wa Uingereza kuhusu kuiuzia silaha Saudi Arabia

Baada ya serikali ya Uingereza kuandamwa na ukosoaji kutokana na hatua yake ya kuiuzia silaha Saudi Arabia na kisha Riyadh kuzitumia silaha hizo kuwaulia wanawake na watoto wa Yemen, Matthew Rycroft balozi na mwakilishi wa Uingereza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amejitokeza na kusema kuwa, nchi yake inafuatilia kwa makini jinsi silaha ilizouuzia utawala wa Aal Saud zinavyotumika.

Akijibu swali la mwandishi wa habari, Matthew Rycroft ameongeza kusema kuwa: Uingereza ina sheria madhubuti kwa ajili ya kudhamini utumiaji unafaa wa kila silaha ya nchi hiyo inayouzwa, hivyo kwa msingi huo basi, silaha ilizouziwa Saudia  pia tunafuatilia kwa makini matumizi yake.

Uhusiano wa madola ya Magharibi na  Saudia kinara wao akiwa Marekani na Uingereza na kunyamzia kwao kimya mauaji ya wanawake na watoto wa Yemen yanayofanywa kwa kutumia silaha za madola hayo ni mfano wa wazi kabisa wa undumakuwili na urongo wa wazi wa madai ya madola hayo ya kutetea haki za binadamu.

Endapo tutajaalia kwamba, madai yote ya Saudi Arabia ya kuhalalisha mashambulio yake ya mabomu huko Yemen na kuwauwa wanawake na watoto wadogo ni ya kweli, je kuiuzua silaha Riyadh na silaha hizo kutumika kuwauwa wananchi wasio na hatia wa Yemjen ni jambo linalokubalika? Kitu kinachopaswa kupewa kipaumbele ni nini? Je, uvamizi na kutaka ukubwa utawala wa Aal Saud nchini Yemen ndio jambo muhimu zaidi au ni roho za mamilioni ya watu wasio na hatia? 

Nyumba nyingi za raia zimebomolewa kufuatia hujuma ya kijeshi ya Saudia 

Umoja wa Mataifa na asasi zilizoko chini ya umoja huo zimetoa ripoti mara kadhaa zinazoonyesha kuwa mbaya hali ya kibinadamu huko Yemen. Katika ripoti ya hivi karibuni kabisa, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia umewekwa katika orodha nyeusi ya nchi zinazoua watoto katika vita au zinazowakata viungo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ni kuwa,  zaidi ya wa 8530, wameauawa katika hujuma ya kijeshi nchini Yemen asilimia 60 wakiwa ni raia na wengine 48,800 wamejeruhiwa tangu Machi 2015 wakati Saudia na washirika wake walipoanzisha hujuma kubwa ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Aidha ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, mashambulio hayo ya kijeshi yamewafanya raia milioni 20 na laki saba wa Yemen wawe ni wenye kuhitajia misaada ya kibinadamu.

Katika ripoti nyingine, William Lacy Swing, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri la Umoja wa Mataifa alitahadharisha  juu ya kuwa mbaya zaidi hali ya kibinadamu nchini Yemen baada ya kuitembelea nchi hiyo na kutoa wito wa kuandaliwa mazingira ya kupatiwa zaidi misaada ya kibinadamu raia wa nchi hiyo. Mkurugenzi Mkuu huyo wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri la Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, mfumo wote wa afya nchini Yemen umesambaratika na kwamba, kuchafuka maji kumepelekea kuibuka maradhi kama kipindupindu ambayo ni vigumu kukabiliana nayo. 

Saudia imeweka kando ubinadamu na kuendelea kuwaua kinyama wananchi wa Yemen

Ripoti yake hiyo inaeleza pia kwamba, raia milioni 21 wa Yemen sio tu kwamba, wanakabiliwa na hatari ya kukumbwa na maradhi ya kipindupindu, bali ili waokoke na hatari ya kifo inayowajongea, wanahitajia misaada ya haraka ya kibinadamu.

Kwa hakika, takwimu hizi zinaeleza kwa uwazi hali mbaya ya kibinadamu inayoikabili Yemen ikiwa ni natija ya siasa za kutaka ukubwa za Saudia huko Yemen. Mwakilishi wa Uingereza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ametetea hatua ya nchi yake ya kuiuzia silaha Saudia licha ya kufahamu hali hii inayotawala nchini Yemen.

Hii ni katika hali ambayo, Jeremy Corbyn kiongozi wa Chama cha Leba cha Uingereza anakiri wazi kwamba, silaha za Uingereza ilizoiuzia Saudia zimekuwa zikitumika kuwaua wanawake na watoto huko Yemen. Ukweli ni kuwa, serikali ya Uingereza, Marekani na madola mengine ya Magharibi ambayo ni wauzaji wa silaha zao kwa Saudi Arabia, ni washirika wa dhambi za mauaji ya wanawake na watoto wa Yemen sambamba na kubomolewa vibaya nchi hiyo masikini na inayohitajia misaada ya kibinadamu.

 

Oct 13, 2017 02:31 UTC
Maoni