• Mwaka 2017, ulikuwa mwaka wa kuendelea kutolewa hukumu za kunyongwa na kupokonywa uraia wananchi wa Bahrain

Jumuiya ya Kitaifa na Kiislamu ya al-Wifaq ya Bahrain ambayo ndio harakati kubwa zaidi ya upinzani nchini humo, imeutaja mwaka 2017 uliomalizika kwamba, ulikuwa mwaka mbaya zaidi kwa upande wa usalama na ukandamizaji wapinzani nchini Bahrain.

Taarifa ya Jumuiya ya Kitaifa na Kiislamu ya al-Wifaq ya Bahrain sambamba na kuashiria kuendelea mauaji dhidi ya wapinzani nchini humo katika mwaka uliopita wa 2017, imebainisha kuwa, katika mwaka huo pia kulishuhudiwa kuendelea kutolewa hukumu za kunyongwa kwa makundi raia wa nchi hiyo na vile vile karibu wanaharakati wengine wa kisiasa wanaokaribia 1000 walitiwa mbaroni katika mwaka huo uliomalizika. Harakati ya al-Wifaq imetangaza kuwa pia kwamba, katika mwaka huo utawala wa kifalme wa Bahrain uliwapokonya uraia wanaharakati 150 wa nchi hiyo. 

Ripoti mbalimbali zinabainisha kwamba, katika mwaka uliopita wananchi wa Bahrain kama ilivyokuwa katika miaka iliyotangulia walikabiliwa na ukandamizaji na utumiaji mabavu mkubwa uliofanywa na utawala wa Aal Khalifa. Kwa hakika wananchi wa Bahrain wanauanza mwaka huu mpya wa 2018 ambapo utawala wa Aal Khalifa ukitumia fursa ya kimya cha jamii ya kimataifa na uungaji mkono wa kila upande wa madola ya Magharibi hususan Marekani umo katika harakati za kushadidisha ukandamizaji dhidi ya wananchi wa nchi hiyo.

Vikosi vya uusalama vikikabiliana na waandamanaji nchini Bahrain

Mark Jones mtaalamu wa masuala ya Mashariki wa nchini Uingereza anasisitiza kuwa: Uungaji mkono wa Rais Donald Trump wa Marekani kwa tawala za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi unaongeza hatua za ukandamizaji dhidi ya wapinzani katika nchi hizo. Urafiki wa Trump na tawala za Saudi Arabia na Bahrain umezifanya nchi hizo ziongeze hatua zao za uvamizi na ukandamizaji.

Hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kukiuka pakubwa haki za binadamu na kuyakandamiza matakwa ya wananchi wa Bahrain imeigeuza nchi hiyo na kuwa gereza kubwa. Utawala huo ukiwa na lengo la kuzima malalamiko ya wananchi wa nchi hiyo umewatia mbaroni wanaharakati wengi na kuwahukumu vifungo vya muda mrefu jela baada ya kuwabambikizia kesi mbali mbali.

Nchini Bahrain harakati za kisiasa za aina yoyote ile zimepigwa marufuku. Aidha utawala huo umepasisha sheria ambazo lengo lake ni kuandaa mazingira ya kukanyaga kikamilifu haki za kisiasa za wananchi. Katika mazingira kama haya, hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kupasisha sheria inayojulikana kama ya kupambana na ugaidi, lengo lake ni kuzidisha ukandamizaji na kushadidisha siasa za kipolisi katika nchi hiyo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi.

Vikosi vya usalama Bahrain vikimtia mbaroni mmoja wa waandamanaji

Kwa mujibu wa vyanzo vya haki za binadamu ni kuwa, Bahrain ikiwa nchi ndogo kabisa ya magharibi mwa Asia ndio nchi yenye wafungwa wengi zaidi wa kisiasa. Natija ya ukandamizaji wa utawala wa Aal Khalifa imeifanya idadi ya wafungwa wa kisiasa katika nchi hiyo kupinduukia elfu nne. Kutiwa mbaroni kiholela wanaharakati wa kisiasa nchini Bahrain na kuhukumiwa adhabu kubwa kama kunyongwa bila shaka kunakinzana wazi na kipengee nambari 10 cha hati ya kimataifa ya haki za binadamu na kipengee nambari 6 cha mkataba maalumu wa haki za kiraia na kisiasa. Aidha kupokonywa uraia ni jambo ambalo linapingwa na mikataba ya kimataifa. Kwa mfano kipingee nambari 15 cha Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu kinasema kuwa: Watu wote wana haki ya kuwa na uraia na hairuhusiwi kujichukulia hatua kiholela na kumpokonya mtu uraia wake. 

Uamuzi wa utawala wa Aal Khalifa wa kuwapokonya uraia wapinzani hususan viongozi wa dini na wa kisiasa ni ukiukaji wa wazi wa haki za awali na za kimsingi za mtu. Hatua hiyo inamnyima pia mtu fursa na haki nyingine za kiraia kama kupiga kura. Ukweli wa mambo ni kuwa, utawala wa kifamilia wa Bahrain umekuwa ukitumia kila wenzo uwe ni wa kisiasa au njama mbalimbali ili sambamba na kuzima harakati ya wananchi, uwatoe kikamilifu wapinzani  katika ulingo wa siasa na uga wa harakati za kijamii nchini humo.

 

Tags

Jan 03, 2018 04:00 UTC
Maoni