• Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Hotuba iliyotolewa Jumapili iliyopita na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA imeonesha tena kwamba, sera za Mfumo wa Kiislamu wa Iran zimebuniwa kwa msingi wa mantiki na busara na kwa kutilia maanani tajiriba na utambuzi wa kina wa malengo ya Marekani.

Jumapili iliyopita Ayatullah Ali Khamenei ambaye alikuwa akihutubia maelfu ya wananchi wanamapinduzi wa Tabriz, mji ulioko kaskazini magharibi mwa Iran aliashiria tabia ya kukiuka makubaliano ya Marekani na uovu wa viongozi wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na kusema: "Tumeona matokeo ya kutegemea maajinabi katika kadhia ya nyuklia ya JCPOA, na tuliwaamini maajinabikatika mazungumzo ya nyuklia lakini hatukupata faida yoyote." 

Msimamo wa Iran wa kutoiamini Marekani si nara na kaulimbiu tupu bali unategemea tajiriba na uzoefu wa miaka iliyopita, mwenendo wa sasa wa watawala wa nchi hiyo na uchambuzi yakinifu kuhusu malengo ya kibeberu ya serikali ya Washington. Ukweli ni kwamba, makubaliano ya nyukllia ya JCPOA hayakuweza kufikia malengo yake kutokana na vizingiti na ukiukaji wa Marekani, suala ambalo sasa limekuwa dukuduku la kimataifa na limezusha wasiwasi mkubwa. 

Imepita miezi 25 sasa tangu makubaliano hayo yalipoanza kutekelezwa huku walimwengu wakiendelea kushuhudia tabia ya Marekani ya kukiuka makubaliano iliyoyatia saini. Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaendelea kusubiri ahadi hewa zilizotolewa na kuharibu wakati na nguvu zake bure bilashi. Suala lenye umuhimu kwa leo na kesho ya taifa la Iran ni kutumia uwezo wa ndani ya nchi hususan sekta na nyanja mbalimbali za kiuchumi. Kama alivyosema Ayatullah Khamenei kwamba: "Mapinduzi ya Kiislamu hayapasi kusimama kwa sababu ya ahadi hewa na njozi."

Ayatullah Ali Khameeni

Mienendo ya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya hususan Ufaransa imepita maudhui ya nyuklia na sasa nchi hizo zimeingilia sekta ya ulinzi ya Iran, na suala hili lina maana ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi huru na kutumia mabavu na dhulma, na lengo lake ni kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu kutokea ndani ya nchi. Dokta Murad Enadi ambaye ni mchambuzi wa siasa na mahusiano ya kimataifa ameandika katika tahariri ya gazeti la Jame Jam linalochapishwa mjini Tehran kwamba: "Japokuwa Donald Trump amesaini hati ya kusitisha vikwazo dhidi ya Iran, na Marekani haijajiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini ameyafanya makubaliano hayo yasiwe na maana kutokana na siasa zake zinazotekelezwa hatua kwa hatua. Katika mchezo wa ping pong unaofanyika baina ya Kongresi ya Marekani na Ikulu ya White House kwa ajili ya kuua makubaliano hayo, Marekani imefadhilisha kuzidisha vikwazo visivyo na mfungamano na masuala ya nyuklia dhidi ya Iran na hivyo kudumisha stratijia ya kiuwekea vikwazo na mshinikizo Tehran. Marekani ambayo imekuwa ikitekeleza vikwazo vilivyopasishwa na Kongresi ya nchi dhidi ya Iran tangu karibu miaka 40 iliyopita, imedumisha na kuimarisha zaidi vikwazo hivyo kwa sera zake mpya kwa kutumia visingizio vya ukiukwaji wa haki za binadamu na madai kuwa Iran inaunga mkono ugaidi."

Trump amesaini vikwazo vipya dhidi ya Iran

Hapa linajitokeza swali kwamba, je haya ndiyo matakwa yote ya Marekani kwa Iran? Jibu la swali hili liko wazi. Marekani haitaki isipokuwa kulidhibiti tena taifa la Iran.

Mwaka mmoja uliopita Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alihutubia taifa na kusema: "Makubaliano haya ya nyuklia ya JCPOA kwetu sisi ni mfano na tajiriba…. Wanatoa ahadi za dhahiri na kuzungumza kwa kutumia maneno matamu na laini lakini katika vitendo wanatekeleza njama za aina mbalimbali, wanafanya uharibifu na kuzuia utendaji wa kazi."

Pamoja na hayo yote Marekani inapaswa ijifunze kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itachagua njia inayodhamini maslahi yake, na itakabiliana na Washington kwa mujibu wa siasa na sera za nchi hiyo kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.   

Feb 20, 2018 04:50 UTC
Maoni