• Russia yatumia kura ya veto kupinga taarifa ya kulaani jaribio la kombora la Korea Kaskazini

Russia imetumia kura yake ya turufu kuzuia kupitishwa taarifa iliyopendekezwa na Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani majaribio ya makombora yanayofanywa na Korea Kaskazini.

Duru za kidiplomasia katika Umoja wa Mataifa zimetangaza leo kuwa Russia imetumia kura ya veto kupinga kupitishwa taarifa iliyoandaliwa na Marekani ambayo inasisitiza kuwa Korea Kaskazini isiwe na haki ya kufanya majaribio mengine mapya ya silaha za nyuklia. Hadi sasa Korea Kaskazini imeshafanya majaribio matano ya silaha hizo. Wiki iliyopita wachambuzi walitahadharisha kuwa eneo la majaribio ya silaha hizo nchini humo limeshawekwa tayari kwa ajili ya jaribio jengine la sita.

Taarifa ya Marekani iliyopigiwa kura ya veto na Russia ilikuwa imeridhiwa na kuidhinishwa na wanachama wengine wote 14 wa Baraza la Usalama ikiwemo China ambayo ni muitifaki mkuu wa Korea Kaskazini.

Jaribio la makombora matatu ya balastiki lililofanywa na Korea Kaskazini

Hii ni katika hali ambayo, jeshi la Korea Kusini lilitangaza mapema kuwa Korea Kaskazini imefyatua kombora kutoka bandari ya Sinpooo katika pwani ya mashariki ya nchi hiyo.

Serikali ya Marekani imekuwa kila mara ikiitaka kila Korea Kaskazini isitishe majaribio yake ya kijeshi na ya silaha za nyuklia. Hata hivyo Pyongyang imeshasisitiza mara kadhaa kuwa itaendelea kuimarisha nguvu na uwezo wake wa kijeshi na wa kujilinda maadamu Washington na waitifaki wake wanaendelea kutoa vitisho dhidi ya nchi hiyo.../

 

Apr 20, 2017 06:57 UTC
Maoni