• Russia yatuma jeshi lenye silaha nzito katika mpaka wake na Korea Kaskazini, hali yazidi kuwa tata

Gazeti la Telegraph la nchini Uingereza limeandika kuwa, Russia imetuma wanajeshi wake wenye silaha nzito katika mpaka wake na Korea Kaskazini kufuatia kuongezeka uwezekano wa Marekani kuivamia kijeshi Korea Kaskazini.

Gazeti hilo limevinukuu vyombo vya habari vya Russia vikisema kuwa, msafara mkubwa wa kijeshi wa nchi hiyo hivi sasa unaelekea kwenye maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo, yaani kwenye mpaka wake na Korea Kaskazini.

Gazeti hilo limeongeza kuwa, picha zilizosambazwa na mtandao wa DVHab.ru wa Russia zinaonesha treni nzima iliyo na zana za kijeshi ukiwemo mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya makombora ikielekea upande wa Vladivostok, mji ulioko katika mpaka wa nchi hiyo na Korea Kaskazini.

Mgogoro baina ya Korea Kaskazini na Marekani umeongezeka katika wiki za hivi karibuni hususan baada ya Korea Kaskazini kufanyia majaribio kombora lake la balestiki.

 

Hivi karibuni Marekani ilituma manuwari zake za kivita kwenye Bahari ya Korea. Hatua hiyo iliyofanyika kwa amri ya moja kwa moja ya Rais Donald Trump wa Marekani imezusha makelele makubwa ulimwenguni.

Hali katika eneo hilo imekuwa ya hatari sana hivi sasa kutokana na siasa za kiuadui na chokochoko zinazofanywa na Marekani dhidi ya ya Korea Kaskazini bila ya sababu yoyote.

Marekani mara kwa mara imekuwa ikisema kuwa, Korea Kaskazini haina haki ya kujiimarisha kijeshi na wala kufanyia majaribio silaha zake. Hata hivyo Korea Kaskazini inasema itaendelea kuimarisha nguvu zake za kijeshi hadi pale Marekani na waitifaki wake watakapoacha uadui wao dhidi ya Pyongyang. 

Apr 21, 2017 04:10 UTC
Maoni