• Watoto wahajiri 150 waaga dunia katika bahari ya Mediterania

Watoto wahajiri zaidi ya 150 waliokuwa wakielekea Ulaya wameaga dunia katika bahari ya Mediterania.

Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) leo Ijumaa umetangaza kuwa katika muda wa miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu wa 2017, vita na migogoro ya kiuchumi hususan katika bara la Afrika na Mashariki ya Kati vimesababisha kupoteza maisha katika bahari ya Mediterania watoto zaidi ya 150 ambao walikuwa safarini kuelekea Ulaya.

Watoto wakimbizi wakijaribu kujiokoa katika bahari ya Mediterania 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tangu kuanza mwaka huu wa 2017 hadi hivi sasa, raia elfu 37 wa nchi za eneo la Mashariki ya Kati na Afrika wamefanikiwa kupata hifadhi nchini Italia kwa kutumia njiai ya bahari, huku asilimia 13 wa wahajiri hao wakiwa ni watoto. Ripoti rasmi zinaeleza kuwa,  jumla ya wahajiri 849 wameaga dunia kwa kuzama majini katika bahari ya Mediterania tangu mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu.  

Afshan Khan, Mkurugenzi wa kikanda wa Shirika la Unicef na Mratibu Maalumu wa Masuala ya Wakimbizi anayeshughulikia masuala ya uhajiri barani Ulaya amesema kuwa, anatiwa wasiwasi na hali ya kusikitisha ya maelfu ya watoto katika njia hiyo ya bahari na ametoa wito wa kubadilishwa siasa zinazohusiana na masuala ya wahajiri wanaoelekea Ulaya hususan katika nchi za pambizoni mwa bahari ya Mediterania ili kuzuia maafa zaidi ya watoto. 

Apr 21, 2017 16:08 UTC
Maoni