Waislamu wa nchini Uingereza wangali wanakabiliwa na vitendo na mashambulizi ya kibaguzi na kigaidi katika sura mpya kutoka makundi ya mirengo ya kulia yenye misimamo mikali. Jinai mpya ya hivi karibuni ilitekelezwa usiku wa Alhamisi ambapo Waislamu watano walimwagiwa tindikali usoni.

Waislamu hao watano walimwagiwa tindikali katika matukio matano tofauti ya kibaguzi. Nukta ya kuzingatia kuhusu jinai hiyo ni radiamali iliyotolewa na vyombo vya habari vya Uingereza khususan Shirika la Utangazaji la nchi hiyo BBC kikiwa chombo muhimu zaidi na kikuu cha upashaji habari cha nchi hiyo. Shirika la BBC halikuzungumza chochote kwamba matukio hayo matano ya kumwagiwa tindikali Waislamu watano ambayo yalitekelezwa kwa nayakati tofauti  huko Uingereza yalikuwa ni mashambulizi ya kigaidi na ya kibaguzi. Bali kinyume chake BBC iliashiria historia ya vitendo vya kumwagiwa tindikali watu katika nchi nyingine na kujaribu kuonyesha kuwa matukio hayo machungu ya kumwagiwa tindikali Waislamu ni jambo la kawaida ambalo lilifanywa na vijana kadhaa wezi.  

Msemaji mmoja wa polisi ya London amesema baada ya Mwislamu mmoja kumwagiwa tindikali kwamba, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa kuna uwezekano kwamba, wavamizi waliwamwagia tindikali madereva wa huduma  za usafirishaji wa vifurushi ili kuwaibia pikipiki au magari yao. 

Wakati huo huo ripoti nyingine ya polisi ya Uingereza imedai kuwa hakuna nyaraka zozote zinazothibitisha kuwa mashambulizi hayo yanatekelezwa kwa malengo ya kibaguzi au kidini. Hata hivyo Jameel Muhktar mmoja wa wahanga wa kumwagiwa tindikali amesema kuwa kile kilichotokea kina mfungamano na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu. Muhktar ameongeza kuwa nchi nzima ya Uingereza ingekusanyika kama raia mwenye asili ya nchi hiyo angeathiriwa na shambulio la aina hiyo na wakati huo huo tukio hilo kutajwa kuwa ni shambulio la kigaidi.  

Wahanga wa shambulio la kumwagiwa tindikali eneo la East London Uingereza

Katika wiki za hivi karibuni kumeripotiwa pia matukio mengine ya kumwagiwa tindikali wanawake wa Kiislamu waliovalia vazi la hijabu. Hata hivyo vitendo hivyo vya jinai havikuakisiwa katika vyombo vya habari vya Uingereza au katika nchi nyingine za Ulaya. Hakuna shaka kuwa wimbi kubwa la propaganda lingetawala kote Uingereza na matukkio hayo kuarifishwa kuwa ni  ya kigaidi iwapo wahanga wa kumwagiwa tindikali hivi karibuni nchini humo wasingekuwa Waislamu. Radiamali inayoonyeshwa na vyombo vya habari na idara za usalama na intelijinsia  za Uingereza kwa shambulio au katika kuamiliana na mijumuiko ya Waislamu baada ya Sala huko London au ile iliyooonyeshwa na vyombo hivyo huko Manchester katika wiki kadhaa zilizopita na pia kuhusu matukio ya kumwagiwa tindikali Waislamu hivi karibuni; yote hayo yanathibitisha wazi jambo hilo. 

Wakazi wa London wakipinga mashambulizi na vitendo vya kibaguzi dhidi ya Waislamu  na wahajiri

Kuna zaidi ya Waislamu milioni tatu wanaounda jamii ya watu wa Uingereza. Waislamu hao hivi sasa wamekumbwa na vizuizi na mibinyo mingi baada nchi hiyo kuamua kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Mashambulizi ya kumwagiwa tindikali Waislamu nchini humo hivi karibuni pia yamezidisha hofu na wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii hiyo. Fikra hii imekuwa ikidhihirishwa na duru za kisiasa na upashaji habari za Uingereza kwamba Uislamu ni dini inayoeneza vitendo vya utumiaji mabavu na misimamo mikali. Fikra hiyo na propaganda zinazoenezwa katika uwanja huo ndizo zinazozua anga ya kupigwa vita dini hiyo na kudhihirishwa kuwa ni tishio nchini Uingereza na katika nchi nyingi za Ulaya. Kwa upande mmoja, serikali ya Uingereza ina mahusiano ya kistratejia na makubwa na nchi ya Saudia ambayo ni muungaji mkono wa makundi yenye misimamo mikali, yenye kueneza machafuko na kuchafua sura ya dini tukufu ya Uislamu yenye kupenda amani na uadilifu. Katika upande wa pili, nchi hiyo inajinadi kuwa mbeba bendera ya mapambano dhidi ya makundi yenye misimamo ya kufurutu ada huku ikiyataja mafundisho ya Kiislamu kuwa ni yenye kufurutu ada na hivyo kuifanya hali ya kisiasa, kijamii na hata kiuchumi kwa Waislamu kuwa ngumu zaidi. Waislamu nchini Uingereza wanapasa pia kuwa na wasiwasi na mashambulizi ya kibaguzi ya mrengo wa kulia ulio dhidi ya Uislamu licha ya kukabiliwa na hali hiyo ngumu ya maisha.

Jul 16, 2017 04:14 UTC
Maoni