• Upinzani dhidi ya uingiliaji wa Marekani katika masuala ya Afghanistan

Wabunge kadhaa wa Bunge la Afghanistan wameyataja matamshi ya balozi mdogo wa Marekani mjini Kabul, Afghanistan kuhusu kesi inayomkabili Jenerali Abdulrashid Dostam, Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi hiyo kuwa ni kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kukiuka mamlaka ya kujitawala nchi ya Afghanistan.

Nasrulah Sadeqi ambaye ni mbunge katika Baraza la Wawakilishi la Afghanistan amesema katika kikao cha wazi cha baraza hiyo kuwa balozi mdogo wa Marekani mjini Kabul hapasi kuingilia masuala ya ndani na ya mahakama za nchi hiyo na kuzusha hitilafu za kisiasa. 

Wabunge wengine wa Bunge la Afghanistan wametaka kukomeshwa uingiliaji wa ubalozi huo wa Marekani katika kesi inayomkabili Jenerali Dostum na kusisitiza kuwa, hakuna nchi yenye haki ya kuingilia masuala ya kisiasa ya Afghanistan. Wamesema mahakama ya nchi hiyo ndiyo inayopaswa kuipatia ufumbuzi kadhia hiyo.

Wabunge wa Afghanistan wamepinga uingiliaji huo wa Marekani katika kesi inayomkabili Jenerali Abdulrashid Dostum Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi hiyo kufuatia msimamo balozi mdogo wa nchi hiyo huko Kabul ambaye ametaka kuchunguzwa kwa makini na kwa uwazi tuhuma  zinazomkabili Jenerali Dostum. 

Uhusiano kati ya Jenerali Dostum na Rais Ashraf - Ghani wa Afghanistan pia  umekumbwa na hitilafu baada ya Ahmad Ishchi mwanachama wa zamani wa chama cha Harakati ya Taifa ya Afghanistan na aliyekuwa Gavana wa Jowzjan kufungua kesi dhidi ya Makamu huyo wa Kwanza wa Rais kwa tuhuma za kumteka nyara na kumtesa mwaka uliopita.  

Ahmad Ishchi, Gavana wa zamani wa mkoa wa Jowzjan nchini Afghanistan

Matamshi ya balozi mdogo wa Marekani mjini Kabul kwamba kesi inayomkabili Makamu wa Kwanza wa Rais wa Afghanistan inapasa kuchunguzwa kwa umakini na kwa uwazi na mahakama ya nchi hiyo ni ishara ya  kuendelezwa siasa za ikulu ya Marekani, White House za kupenda kuingilia masuala ya serikali ya Kabul, uingiliaji ambao umepingwa na wabunge kadhaa wa nchi hiyo.

Wawakilishi wa Bunge la Afghanistan wanaona kuwa kesi inayomkabili Jenerali Dostum ni kadhia ya ndani na kwamba uingiliaji wowote kutoka nje katika suala hilo unakiuka mamlaka ya kujitawala, ya kisheria na kisiasa ya nchi hiyo. Wanasisitiza kuwa suala hilo limazidisha hitilafu za kisiasa huko Afghanistan. 

Jenerali Abdulrashid Dostum, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Afghanistan anayekabiliwa na tuhuma  

hapokuwa katika upande wa pili kesi hiyo iliyowasilishwa na Ahmad Ishchi inalitaja jina la Jenerali Dostum, lakini ofisi ya Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Afghanistan imetangaza mara kadhaa kuwa kesi hiyo imefunguliwa dhidi ya walinzi wa Dostum ambao wanatuhumiwa kuwa walitesa na kuhusika na vitendo vya ubakaji. Hata hivyo inaonekana kuwa Dostum anatuhumiwa kua na mkono wa nyuma ya pazia katika kesi hiyo.  

Aidha siku kadhaa baada ya kufunguliwa mashtaka hayo, Umoja wa Ulaya, Canada, Australia na Norway zilitoa taarifa zikitaka kufanyike uchunguzi rasmi kuhusu tuhuma za haki za binadamu zinazomkabili Jenerali Abdulrashid Dostum. Pamoja na hayo yote kuna mtazamo kwamba hitilafu zilizopo kati ya Rais Muhammad Ashraf-ghani wa Afghanistan, Abdallah Abdallah, Mtendaji Mkuu wa serikali ya Afghanistan na Makamu wa Kwanza wa Rais Jenerali Abdulrashid Dostum, zimetoa fursa kwa madola ya Magharibi kutumia vibaya hali hiyo ili kuingilia masuala ya ndani ya Afghanistan na hasa kesi inayomkabili Dostum. 

Jul 16, 2017 07:55 UTC
Maoni