• Marekani yadai kufuatilia mali zilizoporowa Nigeria katika sekta ya mafuta

Wizara ya Sheria ya Marekani imetangaza kuwasilisha kesi kwa lengo la kuchukua udhibiti wa mali za baadhi ya mashirika na watu katika sekta ya mafuta ya Nigeria wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi.

Marekani inataka kuchukua udhibiti wa nyumba inayogharirmu dola milioni 50 katika mtaa wa matajiri wa Manhattan mjini New York pamoja na meli ya starehe inayogharimu dola miloni 80. Inadaiwa kuwa mali hiyo ilinunuliwa kutokana na fedha zilizopatikana baada ya kuhongwa waziri wa zamani wa mafuta wa Nigeria.

Nyaraka za kesi iliyowasilishwa katika mahakama ya kifiderali ya Houston zinaonyesha kuwa wafanya biashara wawili wa Nigeria walikula njama wakiwa na wengine kumpa hongo waziri Diezani Alison-Madueke, ambaye pia alikuwa anasimamia shirika la kitaifa la mafuta Nigeria.

Baada ya kupokea hongo, Alison-Madueke alihamisha kandarasi zenye faida kutoka tawi la Shirika la Kitaifa la Mafuta la Nigeria na kuzipeleka katika mashirika yanayomilikiwa na wafanya biashara Kolawole Akanni Aluko na Olajide Omokore.

Kwa mujibu wa ripoti mbali mbali, Nigeria ni kati ya nchi zilizo na ufisadi mkubwa kiasi kwamba wakati Mohammadu Buhari alichukua urais wa nchi hiyo mwaka 2015 alitangaza kulipatia kipaumbele suala la vita dhidi ya ufisadi.

Diezani Alison-Madueke

Idara mbali mbali nchini Nigeria zimetumbukia katika kinamasi cha ufisadi na hivi sasa ufisadi huo umekuwa tishio katika sekta za kijeshi na kiuchumi ambapo nchi hiyo sasa inakumbwa na matatizo makubwa ya kiuchumi na katika upande wa pili pia inakabiliwa na ukosefu wa usalama.

Kuna sababu kadhaa ambazo zinatajwa kuwa zimepelekea kuwepo ufisadi Nigeria zikiwemo sababu za kihistoria, kiutamaduni, kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Kwa mtazamo wa kihistoria, ukoloni wa Uingereza nchini Nigeria na uporaji wake wa utajiri wa nchi hiyo ya Kiafrika katika karne iliyopita ni jambo ambalo limeitumbukiza nchi hiyo katika matatizo ya makubwa ya kiuchumi. Wakoloni Waingereza ndio walioingiza tabia ya kupeana na kupokea rushwa nchini Nigeria ili waweze kupata satwa nchini humo.

Mfumo wa kikabila, mapingano ya ndani, ukosefu wa demokrasia, sheria za kibaguzi pamoja na ukosefu wa uadilifu wa kiuchumi na kijamii ni mambo mengine yaliyochangua ufisadi kuenea Nigeria.

Saleh Habib Abdul Raouf, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Nigeria anasema: "Magavana wa kikoloni, na kuwepo mfumo wa kisheria unaowapendelea wanajeshi na wanasiasa wa ngazi za juu, kufichwa nyaraka za umma, kugeuzwa vita dhidi ya ufisadi kuwa uwanja wa malumbano ya kisiasa na baadhi ya itikadi za jadi na kishirikina ni mambo ambayo yamechangia kufeli vita dhidi ya ufisadi nchini Nigeria na maeneo mengine ya Afrika."

Rais Buhari wa Nigeria

Ingawa kadhia ya ufisadi Nigeria si mpya lakini sasa wakuu wa Washington wanaonekana kuibua suala la kuchukua udhibiti wa baadhi ya mali zilizopatikana kwa ufisadi Nigeria ambazo ziko Marekani. Ni wazi kuwa Marekani inafuatilia malengo yake binafsi na wala haina nia ya kuwasaidia watu wa Nigeria katika hatua inazochukua. Itakumbukwa kuwa miaka kadhaa iliyopita waziri mkuu wa wakati huo wa Uingereza alikiuka nidhamu za kidiplomasia na kuitaja Nigeria kuwa nchi iliyozama katika ufisadi. Kauli hiyo ilimkasirisha sana Rais Buhari ambaye alisema: "Uingereza inapaswa kurejesha fedha zote za ufisadi zilizoporwa Nigeria na kuwekwa katika benki za nchi hiyo."

Kwa hivyo katika upande mmoja tunaona wakuu wa Nigeria wakiwa hawana irada imara ya kupambana na ufisadi na katika upande wa pili kuna uingiliaji wa nchi za Magharibi hasa Marekani  katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Iwapo nchi za Magharibi zitarejesha fedha zote za Nigeria na nchi zingine za Afrika basi hali ya watu wa bara hilo itaboreka na ufisadi kupungua.

Jul 17, 2017 07:06 UTC
Maoni