• Waziri Mkuu wa India: Wahindu waache vurugu kwa sababu ya kuchinjwa ng'ombe, mungu wao

Hatimaye Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amewataka Wahindu waache vurugu na machafuko yanayotokana na kupinga kuchinjwa ng'ombe na kuliwa nyama yake kunakofanywa na jamii ya Waislamu nchini humo.

Modi ameyasema hayo mjini New Delhi, mji mkuu wa India katika kikao na viongozi wa vyama vya siasa vya nchi hiyo ambapo amezitaka serikali za kieneo nchini kukabiliana na Wahindu ambao wanasababisha machafuko nchini kutokana na upinzani wao wa kuchinjwa na kuliwa nyama ya ng'ombe kunakofanywa na Waislamu.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi 

Matamshi hayo ya Narendra Modi, yametolewa katika hali ambayo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, yaani tangu kilipoingia madarakani chama cha Bharatiya Janata ambacho ni chama tawala nchini India, kumeshuhudiwa mashambulizi ya jamii ya Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mipaka kuwalenga Waislamu na watu wa jamii nyingine kwa kile kinachosemwa kuwa ni kupinga kuchinjwa ng'ombe na kuliwa nyama yake. Katika mashambulizi hayo, makumi ya Waislamu wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Sanamu linalowakilisha picha ya ng'ombe anayeabudiwa na Wahindu

Kufuatia mashambulizi hayo dini za wachache na vyama kadhaa vya upinzani nchini India kwa mara kadhaa vimekuwa vikimtaka Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kuzuia mashambulizi hayo ya kibaguzi yanayosababishwa na siasa kali, ambapo hata hivyo serikali kuu haijachukua hatua yoyote ya maana katika uwanja huo.

 

 

Jul 17, 2017 14:02 UTC
Maoni