• Korea Kusini yaipa Pyongyang pendekezo la kufanya mazungumzo mwezi huu ili kupunguza mzozo

Serikali ya Korea Kusini imetoa pendekezo la kufanya mazungumzo na Pyongyang kwa ajili ya kumaliza mzozo wa kimipaka ndani ya mwezi huu.

Suh Choo-suk Naibu Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini ameyasema hayo Jumatatu ya leo wakati akiongea na waandishi wa habari ambapo amesisitizia umuhimu wa kufanyika mazungumzo ya usalama na Korea Kaskazini ili kupunguza migogoro iliyopo katika eneo. Suh Choo-suk ameitaja tarehe ya mazungumzo hayo kuwa ni tarehe 21 ya mwezi huu wa Julai na kwamba mazungumzo hayo yanatakiwa kufanyika katika mipaka ya nchi mbili hizo.

Suh Choo-suk Naibu Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini

Pendekezo la kufanyika mazungumzo ya usalama kati ya mataifa hayo hasimu, linatajwa kuwa ni hatua ya awali ya usuluhishi ya serikali ya Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini kuihusu Korea Kaskazini. Wiki iliyopita, Rais Moon Jae-in alinukuliwa akisema kuwa, kufanyika mazungumzo na Korea Kaskazini kwa ajili ya kumaliza tatizo la silaha za nyuklia na makombora ya balestiki ya Pyongyang ni suala la lazima. Hivi karibuni pia serikali ya Korea Kaskazini ilitangza kuwa, siasa za Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Pyongyang, zimefeli na kuchakaa hivyo Washington inatakiwa ijirekebishe. Serikali ya Korea Kaskazini imekuwa ikisisitiza kuwa, siasa za uhasama za Washington dhidi yake ndio zimelifanya eneo la Peninsula ya Kore kuwa tete.

Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini

Wakati huo huo Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini ametangaza leo kwamba umoja huo umeiwekea serikali ya Korea Kaskazini vikwazo vikali sana kwa kile alichokitaja kuwa ni hatari ya silaha za nyuklia na makombora ya nchi hiyo.

Jul 17, 2017 17:06 UTC
Maoni