• Askari wa Afghanistan waandamana kulaani kitendo cha kuandikwa majina ya Mungu na Mtume katika soksi zao

Mamia ya askari wa Afghanistan wameandamana wakilalamikia na kulaani kitendo cha kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu mjini Kabul, mji mkuu wa nchi hiyo.

Taarifa kutoka Kabul zinaarifu kwamba, maandamano hayo ya askari yameshuhudiwa katika kituo cha mafunzo ya kijeshi ambapo askari hao wamelaani kitendo cha kuandikwa jina la Mwenyezi Mungu na Mtume Muhammad (saw) katika soksi zao.

Askari wa Afghanistan

Habari zaidi zinasema kuwa, katika maandamano hayo askari hao wamefunga kwa masaa kadhaa barabara kuu ya Kabul iendayo Jalalabad. Dolat Waziri, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan sambamba na kulaani kitendo cha kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu amesema kuwa, wahusika wote wa kitendo hicho watasakwa na kuchukuliwa hatua kali.

Itakumbukwa kuwa, sare za jeshi la taifa la Afghanistan zinaandaliwa na Marekani na soksi zao zimetengenezwa na moja ya shirika linalojihusisha na uandaaji wa mavazi ya kijeshi.

Askari wa Marekani akihudumia mpopi wa mihadarati nchini Afghanistan

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kuendelea kuwepo askari wa nchi za Magharibi hususan Marekani nchini Afghanistan ni sababu kuu ya ongezeko la machafuko na mchafukoge nchini humo. Mbali na kuchochea machafuko, askari wa Marekani pia wanalaumiwa kwa kuhusika na ongezeko la uzalishaji wa mihadarati nchini Afghanistan.

Aug 12, 2017 13:04 UTC
Maoni