• Mamilioni ya wapiganaji wa kujitolea Korea Kaskazini wajiweka tayari kupambana na Marekani

Vyombo vya habari nchini Korea Kaskazini vimeripoti kwamba karibu watu milioni 3.5 wa kujitolea wametangaza utayarifu wao kwa ajili ya kupambana na Marekani vitani.

Gazeti la Rodong Sinmun la nchi hiyo limeandika kuwa, kwa akali watu milioni tatu na nusu wamejiweka tayari kwa ajili ya kujitolea kupambana na Marekani iwapo nchi hiyo itaanzisha vita dhidi ya Korea Kaskazini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kikosi hicho cha kujitolea kinaundwa na raia wa kawaida, wafanyakazi, askari waliostaafu na wanafunzi kwa lengo la kupambana na Marekani.

Kushtadi mgogoro wa Marekani na Korea Kaskazini

Baada ya Rais Donald Trump kutoa vitisho ambavyo havijawahi kushuhudiwa dhidi ya Korea Kaskazini, Pyongyang nayo ilitishia kukamilisha mpango wa kushambulia kwa makombora kambi za kijeshi katika kisiwa cha Guam hadi kufikia katikati ya mwezi huu wa Agosti.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, mgogoro wa eneo la Korea umezidi kushtadi kutokana na siasa za uhasama za Marekani na washirika wake dhidi ya Korea Kaskazini. Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Australia, Malcolm Turnbull ametangaza kuwa, ikiwa Korea Kaskazini itaishambulia Marekani, basi nchi yake itashirikiana na Washington dhidi ya Pyongyang. Malcolm Turnbull ameyasema hayo baada ya Korea Kaskazini kutangaza kuwa ina mpango wa kushambulia kwa kombora kisiwa cha Guam katika bahari ya Pacific ambacho kiko chini ya udhibiti wa Marekani.

Malcolm Turnbull, Waziri Mkuu wa Australia

Uungaji mkono wa serikali ya Canberra kwa Marekani umetangazwa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutishia kwamba, Korea Kaskazini itashuhudia moto na hasura ambazo hazijawahi kushuhudiwa na walimwengu.

Wakati huo huo Paul Keating, waziri mkuu wa zamani wa Australia amepinga vitisho vya Trump na matamshi ya waziri mkuu wa sasa wa nchi hiyo dhidi ya Korea Kaskazini.

Aug 13, 2017 03:48 UTC
Maoni