• Utafiti: Watu wa Japan, Uhispania, Uswisi na Korea Kusini wanaishi maisha marefu

Utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa, wananchi wa Japan, Uhispania, Uswisi na Korea Kusini wanaishi maisha marefu zaidi ikilinganishwa na watu wa maeneo mengine katika pembe mbalimbali duniani.

Utafiti huo unaonyesha kuwa, Wajapani wanaishi kwa wastani wa miaka 83 hadi kufariki dunia. Sababu kubwa inayotajwa kuchangia katika kurefusha umri wa Wajapani ni vyakula vya asili wanavyokula. Viazi vitamu na samaki ni aina ya vyakula vyenye mchango mkubwa. Pia, jamii ya Japan inatajwa kuwa ni jamii imara isiyo na migogoro mingi jambao ambalo linawasaidia kupunguza msongo wa mawazo.

Nchini Uhispania wastani wa kuishi ni miaka 82.8. Kwa mujibu wa utafiti huo, siri kubwa ya kufikia umri huu ni utajiri wa mafuta bora kwa afya ya mwanadamu yaani mafuta ta zaituni na ulaji wa mboga za majani kwa kiasi kikubwa. Jambo jingine ni tabia ya Wahispania ya kupendelea kutembea zaidi kwa miguu na kuendesha baiskeli hata kama wana magari.

Mazoezi yana nafasi katika kujenga afya ya mtu na kumfanya awe na maisha marefu

Nchi nyingine ni Uswisi ambayo ni mojawapo ya nchi tajiri barani Ulaya. Raia wa nchi hii wanaishi kwa wastani wa miaka 81. Wamefanikiwa kufikia wastani huo mkubwa kwa sababu ya huduma bora za afya, usalama wa raia na mali zao na upendo uliotapakaa katika viunga vya nchi hii tajiri.

Wakati huo huo, tafiti za hivi karibuni zinaitaja Korea Kusini kuwa nchi ya kwanza duniani  kwa raia wake kuishi miaka mingi. Wastani wa umri wa kuishi huko Korea Kusini ni miaka 90. Wamefikia wastani huo kwa kupendelea kula vyakula vilivyochachishwa ambavyo inasemekana vinasaidia kupunguza mafuta mwilini, kuongeza kinga ya mwili, na kuzuia kansa. Pia vyakula vya Wakorea vina kiwango kikubwa cha ufumwele (fibre).

Aug 13, 2017 04:03 UTC
Maoni