• Lavrov: Muelekeo wa Marekani wa kupambana na ugaidi ni wa kindumakuwili

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov, amesema muelekeo na mtazamo wa Marekani kuhusiana na ugaidi ni wa kindumakuwili na kubainisha kuwa muungano unaoitwa wa kimataifa wa kupambana na Daesh (ISIS) chini ya uongozi wa Marekani sio tu haupambani na kundi la kigaidi la Jabhatu-Nusrah bali unafanya jitihada pia za kulilinda kundi hilo.

Lavrov ameongeza kuwa Washington inataka kulilinda kundi hilo la kigaidi ili kuweza kulitumia kwa ajili ya kuipindua serikali ya Syria.

Sergei Rudskol, mkuu wa idara kuu ya operesheni za kamandi ya jeshi la Russia naye pia alitangaza hivi karibuni kuwa muungano eti wa kimataifa wa kupambana na Daesh unaoongozwa na Marekani unakwamisha kuangamizwa kundi hilo la kigaidi nchini Syria.

Muungano huo unaodaiwa kuwa ni wa kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) uliundwa wakati wa urais wa Barack Obama kwa madai ya kupambana na magaidi wa Daesh katika nchi za Iraq na Syria.

Hata hivyo ripoti rasmi zinaonyesha kuwa Marekani na washirika wake wa Magharibi na wa nchi za Kiarabu ni miongoni mwa waasisi na waungaji mkono wakuu wa fedha na silaha wa makundi ya kigaidi yakiwemo ya Daesh na Jabhatu-Nusrah.

Magaidi wa kundi la kitakfiri la Jabhatu-Nusrah

Matamshi ya viongozi wa Russia kuhusiana na undumakuwili wa Washington katika suala la kupambana na ugaidi yametolewa katika hali ambayo hivi majuzi aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Henry Kissinger aliionya serikali ya nchi hiyo kuwa itafanya makosa kama italiangamiza kundi la kigaidi la Daesh katika eneo la Mashariki ya Kati. 

Matamshi hayo ya Kissinger anayejulikana kama mshauri muhimu wa sera za nje za Marekani yametafsiriwa kama ushahidi wa wazi wa kuthibitisha undumakuwili wa Washington katika vita dhidi ya ugaidi na kutilia nguvu hoja kwamba Marekani imekuwa ikiyasaidia na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi na kitakfiri likiwemo la Daesh ili kufanikisha malengo ya uwepo wake haramu katika eneo muhimu na hasasi la Mashariki ya Kati…/

Aug 13, 2017 08:10 UTC
Maoni