• Baraza la Usalama UN lapasisha vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha kwa kauli moja vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini baada ya nchi hiyo kufanya jaribio lake la sita la bomu la nyuklia wiki iliyopita.

Azimio hilo lilipasishwa Jumatatu baada ya Russia na China kuafiki mabadiliko yaliyofanyiwa azimio la awali ambalo lilikuwa limependekezwa na Marekani. Hapo awali Marekani ilikuwa inataka Korea Kaskazini iwekewe vikwazo vikali ili isiweze kuagiza mafuta ya petroli lakini Russia na China zilipinga pendekezo hilo. Aidha Beijing na Moscow zimefanikiwa kuzuia pendekezo la Marekani la kumuwekea vikwazo vya kusafiri kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un au kuzuia mali zake.

Katika azimio hilo lililopasishwa na wanachama wote 15 wa Baraza la Usalama, Korea Kaskazini itaruhusiwa kuagiza mapipa milioni mbili tu kwa mwaka ya mafuta yaliyosafishwa. Aidha nchi hiyo itazuiwa kuuza nje ya nchi bidhaa za vitambaa ambavyo huiingizia pato la dola milioni 752 kwa mwaka.

Makombora ya Korea Kaskazini yakifanyiwa majaribio

Balozi wa Italia katika Umoja wa Mataifa amebainisha wasiwasi wake kuhusu taathira mbaya ya vikwazo hivyo kwa watu wa Korea Kaskazini na amaetaka hatua zichukuliwe kuzia jambo hilo.

Ikumbukwe kuwa katika kulalamikia uchochezi wa kijeshi wa Marekani, Japan na Korea Kusini katika Peninsula ya Korea, Korea Kaskazini tokea mwanzo wa mwaka huu imefanya majaribio kadhaa ya makombora ya balistiki.

Vikwazo hivyo vimepasishwa siku moja tu baada ya serikali ya Korea Kaskazini kutangaza kuwa, ikiwa Marekani itaendeleza njama zake ili kuongeza vikwazo dhidi yake katika Umoja wa Mataifa, basi Pyongyang itaizidishia Washington machungu na taabu.

Sep 12, 2017 03:51 UTC
Maoni