• Kikao cha Bodi ya Magavana wa IAEA, Majukumu na Matarajio

Kikao cha Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kilifanyika jana Jumatatu katika makao makuu ya wakala huo mjini Vienna, Austria.

Kikao hicho kilianza kwa taarifa ya utangulizi wa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Yukia Amano ambaye kwa mara nyingine alitangaza bayana kuwa Iran imefungamana na ahadi zake kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia baina yake na madola sita makubwa duniani yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA ambayo yalitiwa saini 14 July mwaka 2015 na kuanza kutekelezwa Januari 2016.

Kwa mujibu wa mapatano ya NPT ya kuzuia uundwaji na usambazwaji wa silaha za nyuklia, kuna maudhui tatu muhimu katika kadhia ya nyuklia ambazo zinapaswa kuzingatiwa katika fremu ya majukumu ya IAEA.

Awali kabisa ni kuangamizwa silaha za nyuklia na pili ni kuzuia usambazwaji silaha za nyuklia huku kukiwa na usimamizi wa kina katika utekelezwaji wa suala hilo. La kusikitisha ni kuwa, IAEA haijafanikiwa katika kuhakikisha nchi zote duniani zinafungamana na nutka hizo mbili muhiumu za mkataba wa NPT. Hivi sasa si tu kuwa silaha za nyuklia hazijaangamizwa, bali hata Marekani, na wamiliki wengine wa silaha za nyuklia wanaunda kizazi kipya cha silaha hizo za maangamizi ya umati.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Yukia Amano

Nukta ya tatu katika mkataba wa NPT inasisitiza kuwa IAEA inapaswa kusaidia na kuhimiza utumizi wa teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani. La kusikitisha hapa ni kuwa IAEA imekuwa ikifanya mapendeleo  katika uga huu kutokana na kuathiriwa vibaya na malengo ya kisiasa.

Usalama wa nyuklia ambao pia ni kati ya majukumu ya IAEA ni nukta nyingine ambayo imepewa umuhimu katika kikao cha msimu cha bodi ya magavana wa wakala huo wa Umoja wa Mataifa wa nishati ya nyuklia.

Aghalabu ya nchi wanachama wa IAEA hasa nchi zinazostawi zinataka msaada wa wakala huo katika usalama wa shughuli zao za nyuklia. Aidha  IAEA  inapaswa kutoa mafunzo ya kitaalamu na kiufundi katika uga wa nyuklia na taaluma husika.

Kikao cha msimu wa Bodi ya Magavana wa IAEA pia kinajadili wasiwasi wa jamii ya kimataifa kuhusu kuenea na kusambaa silaha za atomiki duniani. 

Katika uga huu, kikao hicho kimejaili hatua ya utawala haramu wa Israel kuwa mmiliki pekee wa silaha za atomniki katika eneo la Mashariki ya Kati.

Ridha Najafi, mwakilishi wa Iran katika IAEA kwa mara nyingine ametoa wito kwa wakala huo wa Umoja wa Mataifa kuondoa wasi wasi kuhusu suala hili.

Kituo cha nyuklia cha utawala wa Kizayuni wa Israel

Utawala wa Kizayuni wa Israel haujajiunga na mkataba wowowote wa kimataifa wa kuzuia uundwaji, umiliki au urundikaji wa silaha za nyuklia. Aidha IAEA haihusiki hata kidogo katika kukagua shughuli za nyuklia za utawala wa Kizayuni wa Israel. Maudhui zote zilizotajwa zina umuhimu wa kipekee na haipaswi kuwepo mapendeleo katika ufuatiliaji wa masuala ya nyuklia.

Takwa la Iran na wanachama wengine wa IAEA ni kuwa nchi zote zinapaswa kufugamana na mikataba ya kimataifa ili malengo ya kimataifa yaliyoainishwa yaweze kufikiwa. Kati ya malengo hayo ni kuhitimisha wasiwasi kuhusu kuenea silaha za nyuklia na kuimarishwa ushirikiano wa kimataifa katika utumizi wa  teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani.

Sep 12, 2017 07:08 UTC
Maoni