• Unyanyasaji watoto wakimbizi wa Kiafrika barani Ulaya

Katika hali ambayo, wimbi la wahajiri wa Kiafrika wanaoelekea barani Ulaya lingali linaendelea kushuhudiwa, ripoti za kimataifa zinaonyesha juu ya kuweko hali mbaya wanayokabiliwa nayo wahajiri hususan watoto wakimbizi wa Kiafrika.

Ripoti zilizotolewa na taasisi kadhaa za kimataifa zenye itibari zinaonyesha kuwa, watoto wahajiri wa Kiafrika wanaofanya jitihada za kuelekea barani Ulaya wamekuwa wakikabiliwa na matatizo makubwa yakiwemo ya kufanyishwa kazi kwa nguvu, kupigwa na kutusiwa na kutumiwa vibaya kijinsia kuliko watoto wa maeneo mengine ya dunia waliolazimika kuhama makwao na kukimbilia nchi za Ulaya. 

Afshan Khan, Mkurugenzi wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF kitengo cha Ulaya na Asia anaamini kuwa, kuna ukweli mchungu nao ni kwamba, watoto wahajiri wa Kiafrika wakati wanapovuka Bahari ya Mediterenia huwa wahanga wa unyanyasaji, magendo, kupigwa, kutusiwa na hata kubaguliwa na mambo hayo yamegeuka kuwa kitu cha kawaida.

Watoto wahajiri wa Kiafrika

Vita na mapigano ya ndani, machafuko ya kisiasa, mazingira mabaya ya kiuchumi ambayo yamefuatiwa na kupanda gharama za maisha, kutawala umasikini, ukosefu wa ajira, taathira ya mabadiliko ya tabianchi na kutokea janga la ukame katika baadhi ya nchi za Kiafrika na matokeo yake ni kuweko uhaba wa chakula ni mambo yanayotajwa kuwa sababu kuu ya wakazi wa nchi mbalimbali za Kiafrika kuamua kuhajiri na kuelekea barani Ulaya kwa ajili ya kwenda kutafuta maisha mazuri.

Wengi wa wahajiri hao hupitia njia ya Libya na Bahari ya Mediterenia na kukumbana na hatari nyingi wakiwa katika juhudi za kufika katika mipaka ya nchi za Ulaya. Hii ni katika hali ambayo, kujikita magenge ya magendo ya binadamu katika pwani ya Libya na katika mipaka mingi ya nchi za Kiafrika na Ulaya ni jambo ambalo limeyafanya maisha ya wahajiri hao yawe hatarini na watoto wahajiri ndio wahanga wakuu.

Wahajiri wa Kiafrika wakiwa katika Bahari ya Mediterenia njiani kuelekea Ulaya

Kwa hiyo wahajiri hao ni chambo kizuri cha magenge ya magendo ya binadamu. Akthari ya wahajiri hao wamekuwa wakiuzwa na kununuliwa katika nchi mbalimbali na makundi ya kigaidi na yenye kufurutu ada kwa ajili ya kutumiwa katika operesheni za kigaidi na za kujitolea muhanga. Baadhi yao wamekuwa wahanga na viungo vyao kuuzwa.

Hata wale ambao hufanikiwa kuvuka na kukwepa hatari zote hizo na kuwasili barani Ulaya salama salmini, hujikuta wakikabiliwa na matatizo mengine kama unyanyasaji, kutumiwa vibaya kijinsia, kubaguliwa au kutumikishwa kwa nguvu. Yote hayo yanatokea katika hali ambayo, akthari ya nchi zimekuwa zikijigamba kuwa ni watetezi wa haki za watoto.

Licha ya kuwa viongozi wa nchi za Ulaya waliwaahidi viongozi wa Kiafrika kwamba, watatoa misaada ya kifedha na kusaidia kuboresha mwenendo wa ustawi barani Afrika kwa ajili ya kudhibiti wimbi la wahajiri, lakini misaada yote hiyo, nayo imekuwa ni kwa ajili ya kudhamini maslahi ya nchi hizo za Ulaya badala ya kuzisadia nchi za Kiafrika.

Katika uwanja huo, mwishoni mwa mwaka 2015 Mfuko wa Dharura wa Dhamana wa Umoja wa Ulaya kwa ajili ya Afrika ulianza shughuli zake kwa lengo la kufunga njia ya wimbi la wahajiri kuelekea barani Ulaya. Hata hivyo hivi sasa pamoja na kupita zaidi ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake, utendaji wa mfuko huo wa dhamana nao umekuwa ukikabiliwa na ukosoaji.

Baadhi ya wahajiri wakiwa Ulaya 

Kiasi kwamba, asasi isiyo ya kiserikali inayojuliukana kama Action for Global Health (AfGH) imesisitiza katika moja ya ripoti zake kwamba, mfuko huo wa dharura wa dhamana wa Umoja wa Ulaya umeanzishwa ili kutoa majibu ya haraka kwa siasa za Ulaya na sio kwa ajili ya kutoa majibu kwa udharura wa ustawi katika nchi washirika. 

Katika mazingira kama haya inaonekana kuwa, kuangalia upya madola ya Magharibi siasa zao za kupenda vita, uingiliaji masuala ya nchi nyingine na ukoloni na vilevile kufanyika juhudi za kurejesha amani na uthabiti ni miongoni mwa mikakati ambayo asaa ikasaidia kupunguza wimbi la wahajiri wa Kiafrika wanaoelekea Ulaya. Wakati huo huo, kuimarisha sheria na kuweko misaada kwa usalama na uzima wa kimwili na kiroho ni mambo ambayo kwa kiwango fulani yatarejesha usalama wa watoto.

Sep 13, 2017 02:34 UTC
Maoni