• Seneti na Kongresi ya Marekani uso kwa uso na Trump kuhusu ubaguzi wa rangi

Katika hatua ya kuonesha kutorishwa kwake na Rais Donald Trump wa Marekani Kongresi ya nchi hiyo imemtaka kiongozi huyo alaani vikali na waziwazi makundi ya wabaguzi wa rangi na wazungu wanaojitambua kuwa bora na juu ya zaidi ya wanadamu wengine.

Mabaraza yote mawili ya Seneti na Kongresi ya Marekani yamemtaka Trump mbali na kuonesha mshikamano na kutoa mkono wa pole kwa wahanga wa ukatili wa makundi hayo ya wabaguzi wa rangi katika matukio ya mji wa Charlottesville kwenye jimbo la Virginia, ayalaani kwa kuyataja kwa majina makundi yote ya wabaguzi wa rangi kama White Nationalism, White Supremacy, Ku Klux Klan na manazi mamboleo.

Azimio la Kongresi ya Marekani limepasishwa kulalamikia msimamo ya Rais wa nchi hiyo, Donald Trump ambaye alikataa kulaani ukatili uliofanywa mwezi uliopita na makundi ya wabaguzi wa Marekani katika mji wa Charlottesville kwenye jimbo la Virginia ambapo kiongozi huyo alionekana kuwapendelea na kuwatetea wabaguzi wa rangi au kwa uchache kutoa matamshi ya kindumakuwili kuhusu harakati na uhalifu wa makundi hayo.

Wafuasi wa kundi la Ku Klux Klan

Sasa Kongresi ya Marekani imemtaka Trump kuonesha msimamo wa wazi na kulaani hadharani na waziwazi harakati za makundi hayo ya kibaguzi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wanasiasa na wanaharakati wa jamii ya Marekani wana wasiwasi kwamba, mienendo ya kutatanisha na kukinzana ya rais wa nchi hiyo kuhusiana na makundi ya kibaguzi hatimaye hatayapa nguvu na kuyastawisha makundi hayo katika jamii na huwenda kukapelekea kukaririwa matukio kama yale ya Charlottesville katika maeneo mengine ya Marekani.

Kuhusu suala hili Richard Cohen ambaye ni Mkuu wa kituo cha South Poverty anasema: Misimamo ya kibaguzi ya kuwapiga vita wageni ya Rais Donald Trump imewahamasisha wafuasi wa makundi yenye misimamo ya kufurutu mipaka ndani ya Marekani na kuzidisha mienendo ya kikatili ya makundi hayo.

Maandamano ya kupinga ubaguzi na mauaji dhidi ya wamarekani weusi, Marekani

Pamoja na hayo na licha ya mashinikizo yanayofanywa dhidi ya Donald Trump haitarajiwi kwamba, Rais huyo wa Marekani  atakuwa tayari kuchukua msimamo dhidi ya makundi ya kibaguzi kama wanavyotaka wanasiasa wengine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Trump alipata ushindi katika uchaguzi wa rais wa mwaka jana kwa msaada na uungaji mkono wa baadhi ya vinara wa makundi hayo ya kibaguzi na amewapa nyadhifa muhimu serikalini baadhi ya waungaji mkono wa makundi ya kibaguzi kama Stephen Kevin Bannon ambaye alikuwa mkuu wa wanastratijia wa Ikulu ya White House. Bannon na mwenzake, Sabastian Gurka walilazimika kujiuzulu kufuatia machafuko ya makundi ya kibaguzi ya Charlottesville.

Trum na Stephen Kevin Bannon

Hata hivyo inaonekana kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani bado ana mfungamano mkubwa wa kiroho na makundi hayo ya kibaguzi ya mrengo wa kulia na anategemea sana kura za makundi hayo katika uchaguzi ujao.

Ni kwa sababu hizo pia ndiyo maana Trump anaendelea kutekeleza ajenda za makundi hayo ya kibaguzi kama sera za kuwapiga vita wageni na wahajiri, kuwazuia raia wa nchi za Waislamu kuingia nchini Marekani na kufuta mpango wa DACA unaowapa hifadhi wahajiri karibu milioni 1.  

Sep 13, 2017 08:31 UTC
Maoni