•  Watu 22 waaga dunia kufuatia kimbunga cha Irma nchini Marekani

Kimbunga cha Irma kimeuwa watu wasiopungua 22 nchini Marekani, huku watu wasiopungua 12 kati ya hao wakiwa wameaga dunia katika jimbo la Florida. Aidha makumi ya mamilioni ya watu wamebaki bila ya umeme kufuatia kimbunga hicho kikali.

Maafisa nchini Marekani wamesema kuwa watu karibu milioni 9.5  kiwango ambacho ni chini ya nusu ya jamii ya jimbo la Florida hawana umeme na kwamba itachukua muda wa siku kumi au zaidi ili kurejesha kikamilifu huduma hiyo.

Gavana wa jimbo la Florida Rick Scot amesema kuwa ni muhimu kurejesha umeme haraka iwezekanavyo kwa kuzingatia hali ya joto iliyopo. Mbali na kuathiri huko Florida, kimbunga cha Irma kimesababisha kukatika kwa huduma ya umeme huko Georgia, Alabama, Carolina ya Kusini na ile ya Kaskazini.

Maafa ya kimbunga cha Irma katika jimbo la Florida Marekani 

Kimbunga cha Irma ambacho juzi kilihesabiwa kuwa ni tufani ya kitropiki kimetajwa kuwa ni moja ya tufani kubwa za Atlantiki. Kimbunga hicho kimeikumba Marekani karibu wiki mbili baada ya kile cha Harvey kusababisha mafuriko makubwa nchini humo na kuuwa watu karibu 70.

 

Sep 13, 2017 14:56 UTC
Maoni