• EU yaunga mkono kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya JCPOA

Umoja wa Ulaya (EU) umeunga mkono kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Umoja wa Ulaya leo Jumatano umewasilisha taarifa katika kikao cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ukisisitiza kuunga mkono kutekelezwa kikamilifu na pande zote makubaliano ya JCPOA ambayo yameidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Taarifa ya Umoja wa Ulaya imebainisha kuwa umoja huo uko jadi katika kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo ambayo yamepasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Wakati huo huo ripoti ya hivi karibuni ya Yukia Amano Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa IAEA kuhusu Iran pia itachunguzwa katika siku ya tatu ya  kikao cha msimu cha Bodi ya Magavana ya wakala wa IAEA. Yukia Amano alisema juzi Jumatatu wakati wa kuanza kikao cha Bodi ya Magavana kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umethibitisha kwa mara nyingine tena kuwa Iran imefungamana na kutokengeuka mkondo wa makubaliano yaliyofikiwa.

Yukia Amano, Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa IAEA  

Naye David Howell, Mkuu wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa katika Bunge la Uingereza leo amemtumia barua  Boris Johnson, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo akiitaka London ionyeshe uungaji mkono wake wa wazi kwa makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1.  Aidha Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa siku chache zilizopita alisisitiza kuwa nchi yake inaunga mkono kwa mara nyingine tena makubaliano ya JCPOA. 

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa 

 

Sep 13, 2017 14:58 UTC
Maoni