• Radiamali ya Moscow kwa hatua mpya ya Marekani isiyo ya kidiplomasia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa serikali ya Marekani inavuruga uhusiano kati yake na Russia.

Maria Zakharova ameashiria leo katika mkutano na waandishi wa habari hatua ya Marekani ya kuteremsha chini bendera za Russia katika majengo ya kidiplomasia ya nchi hiyo huko Marekani na kueleza kuwa kwa kutekeleza hatua hiyo, Marekani inaharibu pakubwa uhusiano kati yake na Russia. 

Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia 

Zakharova ameongeza kuwa Moscow imewasilisha malalamiko yake makali kuhusu suala hilo kwa viongozi wa Marekani na kwamba inataraji kuchukua uamuzi mkabala na hatua hiyo ya Washington. Serikali ya Marekani hivi karibu iliziteremsha bendera za nchi ya Russia zilizokuwa katika jengo la ubalozi mdogo wa nchi hiyo huko San Francisco na katika ofisi ya mwakilishi wa biashara wa nchi hiyo huko Washington DC kufuatia kufungwa jengo na ofisi hiyo. 

Washington imeiwekea Russia vikwazo vipya vya kidiplomasia na Moscow pia imejibu hatua hiyo ya Marekani kwa kuwafukuza nchini Russia wafanyakazi na wanadiplomasia wa Marekani zaidi ya 750. 

 

Oct 12, 2017 14:03 UTC
Maoni