• John Kerry: Trump anasema uongo kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry ameukosoa vikali msimamo hasi ambao unatazamiwa kutangazwa na rais wa nchi hiyo Donald Trump kuhusiana na makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1.

Kerry amesema: Trump anawaambia uongo Wamarekani kuhusu makubaliano haya ya kimataifa.

Waziri huyo aliyetangulia wa mambo ya nje wa Marekani amesisitiza na kutahadharisha kuwa kujitoa Washington katika makubaliano ya JCPOA ni jambo hatari, lisilo na nadhari na litalosababisha kutengwa nchi hiyo.

Hayo yanajiri huku msemaji wa Ikulu ya Marekani White House Sarah Huckabee Sanders, akitangaza jana kuwa Rais Donald Trump wa nchi hiyo leo saa saba  kasorobo mchana kwa saa za Marekani atatangaza msimamo wa serikali yake kuhusu makubaliano hayo ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

John Kerry (kushoto), Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif (katikati) na Mkuu wa Sera za Nje wa EU Federica Mogherini baada ya kusainiwa makubaliano ya JCPOA

Kwa mujibu wa kanuni zake za ndani, serikali ya Marekani inapaswa kila baada ya siku 90 itoe ripoti kwa Kongresi ya nchi hiyo kuhusiana na kuendelea kuheshimu na kutekeleza Iran makubaliano ya JCPOA. Trump ana muda hadi tarehe 15 mwezi huu wa kuwasilisha  ripoti hiyo kwa Kongresi.

Vyombo vya habari vya Magharibi vimetangaza kuwa kuna uwezekano katika ripoti yake hiyo, Trump hatothibitisha kuwa Iran inaheshimu na kufungamana na makubaliano hayo.

Endapo Rais huyo wa Marekani atafanya hivyo, Kongresi itakuwa na muda wa siku 60 kupitisha uamuzi kuhusu kuiwekea tena Iran vikwazo, ambavyo utekelezaji wake utahitaji kusimamishwa utekelezaji wa JCPOA, na ikiwa itapiga kura ya kurejeshwa na kutekelezwa tena vikwazo hivyo, Marekani itajitoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa ambayo iliyaridhia na kuyasaini kwa pamoja na madola mengine matano ya Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Russia na China.../ 

Oct 13, 2017 07:35 UTC
Maoni