• Msimamo wa Trump dhidi ya makubaliano ya JCPOA, uharibifu wa mkataba wa kimataifa

Akizungumza katika kikao cha Kuisafisha Dunia na silaha za nyuklia mjini Moscow, Russia Abbas Araghchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika Masuala ya Kisheria na Kimataifa sambamba na kukosoa miamala mibovu ya serikali ya Marekani kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA amesema kuwa, misimamo yote ya Rais Donald Trump kuhusu makubaliano hayo ni ya kuharibu mikataba ya kimataifa.

Akiashiria nukta kinzani na miamala mibaya ya Marekani kuhusiana na makubaliano hayo ya nyuklia, Abbas Araghchi amebainisha kwamba, kwa mujibu wa vipengee vya 26, 28 na 29 vya makubaliano ya JCPOA, Marekani iliahidi kuyatekeleza kwa nia njema na kwamba ingejiepusha na kitendo chochote kitakachosababisha kutiwa doa maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwemo kuondolewa vikwazo dhidi ya taifa hili. Hata hivyo hadi sasa Washington haijavifanyia kazi vipengee hivyo, kama ambavyo pia imekiuka ahadi zake kwa mara kadhaa kuhusiana na makubaliano tajwa.

Abbas Araghchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Kukiukwa makubaliano ya nyuklia kunakofanywa na Marekani, ni hatua ambayo imeiletea jamii ya kimataifa changamoto kubwa. Moja ya changamoto hizo, ni kupuuzwa mikataba ya kimataifa suala ambalo linaisababishia hasara kubwa jamii hiyo. Kuhusiana na suala hilo, Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter kwamba: "Wapenda vita wanajaribu kuonyesha wasi wasi kwamba sisi (Iran) tutaweza kuheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Hakuna sababu ya wasi wasi huo. Marekani nayo inatakiwa iheshimu na makubaliano hayo kama vile sisi tulivyoyaheshimu." Mwisho wa kunukuu. Katika safari yake ya kwanza ndani ya eneo la Mashariki ya Kati na kwa lengo la kuchafua anga chanya iliyoletwa na makubaliano hayo kupitia ziara yake nchini Saudia na pia kushiriki kongamano la mjini Riyadh, Rais Donald Trump wa Marekani alijaribu kuiingiza Iran katika mchezo mpya wa mgogoro wa kieneo. Aidha Jumamosi iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Wayne Tillerson alifanya safari nchini Saudia kwa malengo hayo hayo.

Rais Donald Trump wa Marekani

Fayad Zahid, mhadhiri wa chuo kikuu na mwandishi wa habari sambamba na kukosoa mienendo mibaya ya Marekani kupitia mahojiano na Shirika la Habari la IRNA anasema: "Katika eneo la Mashariki ya Kati Marekani inatekeleza siasa za undumaiakuwili. Kwa upande mmoja matamshi yasiyo ya mantiki ya Trump, yamezisababishia nchi za Ulaya na eneo la Mashariki ya Kati aina fulani ya mkanganyiko. Hii ni kwa kuwa haifahamiki ni nini undani wa mienendo na stratijia ya Trump na je inawezekana mienendo hiyo kuaminiwa au la? Pili ni kwamba kando ya mkanganyiko huo wa kisiasa, inaonekana kuwa kukusanyika watu wenye misimamo mikali ndani ya White House huko Marekani, kuna lengo la kuzusha anga ya vita ndani ya eneo na kudhamini maslahi yao binafsi ya kiuchumi sambamba na kudhamini usalama na stratijia ya utawala wa Kizayuni." Mwisho wa kunukuu.

Trump akicheza Dansi na mfalme wa Saudia ambaye ni rafiki yake mkubwa

Aidha msomi mmoja wa mjini Washington ameandika kuhusu malengo yanayofuatiliwa na Marekani katika eneo hili kwamba: "Stratijia mpya za Marekani zimejikita katika kuifuatilia Iran hasa juu ya uwezo wa kijeshi wa nchi hiyo (Iran), kuongezeka ushawishi wake katika eneo, kuyaimarisha makundi ya muqawama na kadhalika kutuma washauri wake wa kijeshi nje ya nchi kwa ajili ya kukabiliana na makundi ya kigaidi." Mwisho wa kunukuu. Ili kuvuruga makubaliano ya nyuklia Marekani inadai kuwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanalipa nguvu jeshi la  Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na katika uwanja huo inajaribu pia kuionyesha Iran ya Kiislamu kwa sura ya ugaidi. Madai kuwa uwezo wa makombora ya Iran ni tishio kwa usalama wa eneo., mafanikio ya Iran ya kukabiliana na kundi la Daesh (ISIS) na makundi mengine ya kigaidi na pia hatua ya Tehran ya kutetea haki za taifa la Palestina dhidi ya utawala vamizi wa Kizayuni ni miongoni mwa mbinu chafu zinazotumiwa na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Oct 23, 2017 02:41 UTC
Maoni