• Stratijia mpya ya ISIS katika awamu ya baada ya kusambaratishwa

Licha ya kumalizwa na kuangamizwa kijeshi genge la kigaidi la Daesh (ISIS) lakini bado hatuwezi kusema kuwa vitendo vyote vya genge hilo la wakufurishaji vimemalizika.

Kukombolewa mji wa al Bukamal huko Deir ez-Zor Syria na mji wa Rawa huko al Anbar Iraq kuna maana ya kuangamizwa kijeshi genge la kigaidi la Daesh lakini hakuna maana ya kumalizika jinai za genge hilo. Kundi hilo la kigaidi limeshindwa katika ndoto zake za kuunda khilafa lakini hapo hapo imeanza awamu mpya ya vitendo vya kundi hilo ambayo ni kama vile kurejea ilikuweko huko nyuma.

Kusambaratishwa magaidi wa Daesh (ISIS)

 

Hivi sasa Daesh haina tena zile nguvu za kuwashawishi watu kama ilivyokuwa mwaka 2014 na baadaye ambapo baadhi ya watu wenye fikra finyu walivutika kujiunga kwa wingi na genge hilo. Mgogoro mkubwa uliolikumba kundi la Daesh hivi sasa ni uchache wa wanachama wake na kupoteza vyanzo vyake vya kifedha. Pamoja na hayo, genge hilo linaendeleza jinai zake kwa shabaha ya kuvuruga tu mambo na kutoruhusu raia waishi kwa usalama na bila ya hofu. Hivi sasa genge hilo halifikirii tena kuteka ardhi na kuunda khilafa yake, bali lengo lake ni kuzusha hofu tu na kujionyesha mbele ya watu kuwa bado lipo.

Katika awamu hii mpya, genge hilo linafanya operesheni za kigaidi na miripuko ya hapa na pale. Si hayo tu lakini pia linatumia mbinu zisizo za kawaida kama vile kuwavamia na kuwakanyaga kwa gari watu kama ilivyotokezea mara kadhaa katika nchi za Magharibi kama vile Marekani na nchini Uhispania. 

Nukta nyingine hapa katika awamu hii mpya ya mashambulizi ya genge la kigaidi la ISIS ni kuwa kundi hilo linafanya mashambulizi yake kwa kutumia vijikundi kadhaa ambavyo tab'an havina mguso sana na wala havina nia ya kuwa na eneo la kijiografia la kiutawala. Mfano wa wazi wa vijikundi hivyo ni kundi la kigaidi lililozuka hivi karibuni nchini Afghanistan na kufanya mashambulizi ya kigaidi nchini humo. Kuna uwezekano pia kwamba kundi la Daesh limefikia mapatano na baadhi ya vijikundi vya kigaidi kuendesha mashambulizi yao katika maeneo tofauti duniani.

Watoto wa Syria wakisherehekea ushindi wa jeshi la nchi yao dhidi ya magaidi wa ISIS

 

Suala jingine ni kwamba kuna uwezekano pia wa kutokea mabadiliko katika maeneo ya kijiografia ya Daesh yaani genge hilo la kigaidi kuhamishia vitendo vyake katika maeneo mengine ya dunia. Ijapokuwa nchi kama Syria, Iraq na Yemen bado ni muhimu kwa genge hilo, lakini vitendo vya kigaidi vya kundi hilo vimepungua katika nchi hizo kutokana na kudhoofishwa sana na sasa limeaamua kuelekeza nguvu zake katika maeneo mengine duniani hasa kaskazini mwa Afrika ikiwemo nchini Libya, Somalia na Nigeria. Inavyoonekana ni kwamba nchi za Kiarabu zinapaswa kuwa na wasiwasi zaidi hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote kwani kuna raia wengi wa nchi hizo waliojiunga na Daesh katika miaka ya hivi karibuni na baada ya kusambaratishwa dola lao waliloota kuliunda katika ardhi za Syria na Iraq, sasa raia hao hawana njia nyingine isipokuwa kurejea walikotoka, wakiwa wameiva kwa fikra za ukufurishaji na za kigaidi tena wakiwa wamepata mafunzo ya kijeshi. Si hayo tu, lakini watu hao wanaugua maradhi ya kisaikolojia kutokana na jinai za kutisha walizoziona na baadhi yao walizozifanya huko Syria na Iraq. Watu hao ni hatari kubwa kwa nchi za Magharibi kwani mara zote wako tayari kutenda jambo lolote lile. Ni kwa sababu hiyo ndio maana wafuatiliaji wa mambo wakasema kuwa, si jambo lililo mbali kuona vinaongezeka vitendo vya kigaidi ya genge la kigaidi la Daesh katika nchi za Magharibi.

Nukta ya mwisho ya kuashiria hapa ni kuwa, genge la kigaidi la ISIS limesambaratishwa kijeshi lakini fikra za Kidaesh na za ukufurishaji bado zipo. Watu wenye fikra hizo bado ni wengi na si katika eneo la Mashariki ya Kati tu, bali pia katika nchi za Magharibi ambazo kimsingi ndizo zilizounda magenge hayo na kuyaunga mkono kifedha na kijeshi ili kuuvuruga ulimwengu wa Kiislamu. Jambo hilo linazidi kutia nguvu tahadhari zinazotolewa za kutokea mashambulio ya kigaidi katika nchi za Ulaya na Marekani.

Nov 23, 2017 12:30 UTC
Maoni