• Saudia inatumia mamluki wa Marekani kuwatesa wanawafalme wanaozuiliwa

Inaarifiwa kuwa, utawala wa Riyadh umekuwa ukiwatumia mamluki waliowakodisha kutoka Marekani katika kuwatesa na kuwakandamiza wanawafalme na wajasiriamali mabilionea wa Saudi Arabia waliokamatwa hivi karibuni katika kile kilichotajwa kuwa wimbi la vita dhidi ya ufisadi.

Tovuti ya habari ya DailyMail.com imeripoti kuwa, mamluki hao wa Marekani wanatumia kila namna ya mateso dhidi ya watuhumiwa hao wa ufisadi. 

Miongoni mwa mbinu hizo za utesaji ni kupigwa, kuzabwa makofi, kutukanwa, kudhalilishwa na kuning'inizwa kichwa chini miguu juu.

Tovuti hiyo imenukuu duru za habari ndani ya Saudia zikisema kuwa, mamluki hao wamekodishwa na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, Mohammed Bin Salman kutoka kampuni binafsi ya usalama ya Marekani iliyojulikana kama "Blackwater-linked" na ambayo kwa sasa inafahamika kama Academi.

Walid bin Talal bin Abdulaziz, bilionea wa Saudia anaezuiliwa

Mapema mwezi huu, utawala wa kifalme wa Saudi Arabia uliwatia nguvuni na kuwaweka kizuizini makumi ya Wanamfalme na mawaziri wa zamani na wa sasa wa utawala huo kwa kisingizio cha kupambana na ufisadi.

Katika orodha ya waliotiwa nguvuni yamo majina ya shakhsia maarufu na wanamfalme ikiwa ni pamoja na Walid bin Talal bin Abdulaziz, bilionea mkubwa zaidi nchini Saudia.

Tags

Nov 23, 2017 14:24 UTC
Maoni