• Indhari ya viongozi wa Pakistan juu ya kusajiliwa shule za kidini zenye mielekeo ya Uwahabi

Naibu Waziri wa Masuala ya Kidini nchini Pakistan, Mohammad Aftab ameonya juu ya kusajiliwa shule za kidini zenye mielekeo ya Uwahabi nchini humo.

Aftab amesema kuwa, kuenezwa Uwahabi katika baadhi ya shule za kidini nchini Pakistan kumepelekea kuongezeka makundi yenye misimamo ya kufurutu ada na ya ugaidi. Naibu Waziri wa Masuala ya Kidini nchini Pakistan, amesema kuwa, kusajiliwa shule za kidini kunatekelezwa kupitia mpango wa kitaifa wa kupambana na ugaidi nchini humo. Hivi karibuni serikali ya Pakistan ilitangaza kwamba, kati ya shule elfu 30 za kidini zinazoendesha shughuli zake ndani ya taifa hilo ni shule elfu 13,400 tu ndizo zilizosajiliwa rasmi ambapo baadhi yake zina mielekeo ya Uwahabi.

Walimu wanaotoa mafunzo ya Kiwahabi katika shule za kidini nchini Pakistan

Baada ya Marekani kuivamia kijeshi Afghanistan mwaka 2001 na hatua ya Pervez Musharraf, rais wa wakati huo wa Pakistan ya kutoa ushirikiano kwa Washington katika uvamizi huo, kwa mashinikizo ya Marekani, kiongozi huyo alichukua hatua kali dhidi ya shule za kidini ambapo baadhi ya hatua hizo ilikuwa ni kuweka uangalizi wa masomo yanayofundishwa katika madrasa hizo. Mbali na hayo ni kwamba serikali ya Pakistan ilitoa amri ya kusajiliwa shule hizo. Sisitizo jipya la serikali ya Islamabad juu ya kusajiliwa kwa shule za kidini, linaonyesha kwamba katika kipindi cha miaka 16 iliyopita shule nyingi za kidini zilikataa kuitikia wito huo wa kusajiliwa.

Pervez Musharraf, rais wa zamani wa Pakistan

Kwa mtazamo wa Marekani, shule hizo ndio chanzo cha kuenea vitendo vya utumiaji mabavu na ugaidi katika eneo na hivyo ikaitaka serikali ya Islamabad iziwekee udhibiti. Ukweli ni kwamba moja ya tofauti zilizopo kati ya Washington na Islamabad ni kuhusiana na usimamizi juu ya utendajikazi wa shule za kidini nchini humo. Kuhusiana na suala hilo, Khadijah Askar, mtaalamu wa masuala ya kisiasa ya Pakistan anasema: "Karibu shule zote za kidini nchini Pakistan zinafadhiliwa na Saudia na akthari ya shule hizo kama vile shule ya 'Madrasatul-Arabiyyah Pakistaniyyah' na 'Darul-Ulum Haqqaniyyah' ni ngome za kutolea mafunzo kwa wapiganaji wa makundi ya kigaidi nchini humo." 

Baadhi ya wanafunzi waliohitimu katika shule za Kiwahabi nchini Pakistan

Kutolewa bure elimu katika shule nyingi za kidini sambamba na kuziwekea mabweni kwa wanafunzi wanaosomea maeneo hayo sambamba na kuwapatia fedha na malazi wanafunzi hao, kumezifanya familia nyingi masikini na za vijijini ziwapeleke watoto wao kwenye madrasa hizo ambazo ni kiini cha mienendo ya misimamo mikali na ya kigaidi. Katika miaka ya hivi karibuni shule hizo zinazoendeshwa kwa bajeti ya Saudia na kutoa mafundisho ya Kiwahabi zimegeuka kuwa eneo la kuenezwa mielekeo ya kufurutu ada katika eneo la Mashariki ya Kati na hivyo kuwa tatizo kubwa hata kwa serikali yenyewe ya Pakistan. Kuhusiana na suala hilo, Daniel Pipes mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Hatua ya Saudia ya kudhamini kifedha shule hizo ni njama ya muda mrefu ya Riyadh ya kuupa nguvu na kuuimarisha Uwahabi duniani. Hadi sasa pia kunaweza kushuhudiwa juhudi hizo katika maeneo mengi ya dunia kuanzia Marekani, hadi peninsula ya Balkan, Afrika, Pakistan na Indonesia.

Magaidi wa Kiwahabi ambao ni matokeo ya mafundisho ya pote hilo la Uwahabi

Katika nchi nyingi, Aal-Saud wanafadhili kwa kiwango kikubwa cha fedha ujenzi wa shule za Kiwahabi, suala ambalo kwa hakika linatia wasi wasi mkubwa." Alaa kulli hal, inaonekana kwamba serikali ya Pakistan chini ya mashinikizo ya Marekani inakabiliwa na hali ngumu kwa ajili ya kuchukua maamuzi kuhusiana na shule za kidini sambamba na kuendeleza mashirikiano na Marekani. Licha ya baadhi ya viongozi wa Pakistan kudai kwamba mashinikizo ya Washington hayana taathira, lakini safari za mara kwa mara za viongozi wa chama tawala cha Muslim League nchini Saudi Arabia zinaonyesha kwamba serikali ya Islamabad inajaribu kufanya mazungumzo na Saudia kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi juu ya uangalizi wa madrasa hizo.

Tags

Jan 02, 2018 04:13 UTC
Maoni