• Upinzani wa vyama vya Uturuki wa kuungana nchi yao na Marekani na Israel

Vyama vya kisiasa nchini Uturuki vimepinga siasa za nchi yao za kuungana na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Temel Karamollaoğlu, mkuu wa chama cha Saadet cha Uturuki amesema: Hatua za siri na za wazi za Marekani na utawala wa Kizayuni ndizo zinazokwamisha ustawi wa nchi yake.

Mwanasiasa huyo Mturuki pia ameonya kuhusu vitendo vya chuki vya utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani dhidi ya nchi yake na kusema: Marekani na Israel haziwezi kuwa waitifaki wa kiistratijia wa Uturuki. Amesema, Marekani inawapa mafunzo na silaha magaidi ambao ni maadui wa Uturuki katika eneo hili lakini pamoja na hayo, serikali ya Ankara inaziona tawala zinazounga mkono magaidi kuwa ni waitifaki wake wa kiistratijia.

Rais Erdogan wa Uturuki (kulia) na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu

 

Licha ya kutoa matamshi hayo dhidi ya chama tawala cha Uadilifu na Ustawi, lakini ni jambo lisilo na shaka kwamba chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha Saadet ni miongoni mwa vyama vinavyounga mkono siasa za chama tawala katika masuala ya ndani bali hata ya nje ya Uturuki. Ijapokuwa hatuwezi kusema kuwa chama cha Saadet kinafanana kikamilifu na chama tawala cha Uadilifu na Ustawi lakini viongozi wa vyama vyote viwili wana misimamo sawa katika masuala tofauti. Miongoni mwa masuala yanayowaunganisha viongozi wa vyama hivyo viwili ni namna wainavyoiangalia Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kabla ya hapo, viongozi wa serikali ya Uturuki wamenukuliwa mara chungu nzima wakiilaani Marekani kwa kuwatumia silaha waasi wa Kikurdi wa Syria na hata kutoa onyo kali kwa viongozi wa White House. Kwa mfano mwezi Mei mwaka ulioisha wa 2017, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki aliionya vikali Marekani na kutishia kulipiza kisasi kutokana na misaada yake ya kijeshi kwa chama cha Kikurdi cha PKK pamoja na misaada yake ya kijeshi na kifedha kwa waasi wa Kikurdi wa Syria wanaojulikana kwa jina la YPG. Wakati huo Erdogan alisema: Uturuki italipiza kisasi kila tone la damu linalomwagwa na silaha za Marekani, na kisasi hicho kitalipizwa dhidi ya watoaji wenyewe wa silaha hizo akiwakusudia Wamarekani. Kwa upande wake, Nurettin Canikli, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki ameituhumu Marekani kwa kutumia kisingizio cha ugaidi kuyapa misaada mikubwa magenge ya kigaidi. Viongozi wa serikali ya Uturuki wamekuwa wakitangaza waziwazi kuwa viongozi wa Marekani ndio waungaji mkono wakuu wa makundi ya Kikurdi. Wanasema, Marekani inawatumia vibaya Wakurdi katika eneo hili kwa ajili ya kufanikisha malengo yake machafu. Kwa upande wake, Musa Qurbaniev, mmoja wa wachambuzi wakubwa wa masuala ya Uturuki wa nchini Azerbaijan anasema:

Nurettin Canikli, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki

 

Magaidi wanaojipa sura ya Kiislamu ni wenzo mkuu unaotumiwa na Marekani kwa ajili ya kutoa pigo kwa ulimwengu wa Kiislamu na kufanya uharibifu mkubwa katika nchi kadhaa za Waislamu.

Mchambuzi huyo wa masuala ya kisiasa wa nchini Azerbaijan aidha amesema:

Viongozi wa nchi za Kiislamu wanapaswa kuwa macho, kwani lengo la Magharibi na hasa Marekani katika kuwaunga mkono magaidi, ni kuzigawa vipande vipande nchi tajiri za Kiarabu na zisizo za Kiarabu katika ulimwengu wa Kiislamu kama vile Uturuki.

Kiujumla tunaweza kusema kuhusu matamshi ya mkuu wa chama cha Saadet cha Uturuki aliyepinga vikali siasa za nchi hiyo za kuungana na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba, katika mwaka uliomalizika wa 2017, Marekani ilitumia magenge ya kigaidi kama vile Daesh (ISIS) na msaada baadhi ya nchi za eneo hili kama Uturuki kuzusha mgogoro mkubwa katika nchi za Waislamu. Cha kushangaza ni kuwa, licha ya viongozi wa Uturuki kukosoa siasa za Marekani katika eneo hili, bado wanaendelea kushirikiana nao na kuwarahisishia njia za kutekeleza siasa zao za kiuadui dhidi ya nchi za Kiislamu za eneo hili.

Jan 02, 2018 06:21 UTC
Maoni