• Watu tisa wauawa katika ghasia ndani ya gereza Brazil

Watu wasiopungua tisa wameuawa na wengine 14 kujeruhiwa katika ghasia zilizotokea jana Jumatatu ndani ya gereza nchini Brazil huku wafungwa zaidi ya 100 wakitoroka.

Taarifa zinasema kuwa wafungwa walivamia eneo la gereza walimo wanachama wa genge hasimu na mapigano yaliyojiri yalipelekea moto mkubwa kuibuka katika Gereza la Jimbo la Goias.

Wazimamoto walifanikiwa kuzima moto huo na kuwakamata wafungwa 29 kati ya 106 ambao walitoroka wakati wa rabsha hizo.

Wafungwa nchini Brazil

Halikadhlika jana Jumatatu wafungwa wengine 10 walitoroka kutoka gereza la Jimbo la Amazonas. Brazil ina wafungwa 726,712 suala linaloifanya ishike namba tatu kwa idadi kubwa zaidi ya wafungwa duniani.

Magereza hayo ya Brazil yana uwezo wa kuwa na wafungwa 368,049 na kwa msingi huo msongamano mkubwa wa wafungwa hupelekea kuibuka mapigano ya mara kwa mara baina ya magenge hasimu.

Tags

Jan 02, 2018 15:10 UTC
Maoni