• Jibu la Wapakistan kwa matamshi mapya ya Trump

Matamshi mapya ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu makosa ya kistratijia ya nchi hiyo katika kuipa Pakistan misaada ya kifedha kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, yamekabiliwa na radiamali kali kutoka kwa Wapakistan.

Jumatatu iliyopita Rais Donald Trump wa Marekani aliandika katika mtandao wake wa Twitter matamshi ya kuishambulia Pakistan kwa kudai kwamba Marekani ilifanya upumbavu mkubwa kwa kuipatia nchi hiyo dola bilioni 33 kwa zaidi ya miaka 15. Kadhalika alidai kwamba, licha ya Marekani kuipatia nchi hiyo kitita chote hicho, lakini Islamabad hakuna ilichokitoa mkabala wa msaada huo ghairi ya uongo na hila. Katika kujibu matamshi hayo ya matusi  na dharau ya Trump, Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imemwita David Hale, balozi wa Marekani nchini humo na kumlalamikia kuhusiana na mienendo hiyo hasi ya Rais Trump. Wanaharakati wa vyama vya siasa nchini humo nao pia wameonyesha hasira zao kutokana na matamshi hayo ya Trump. 

Sherry Rehman, mmoja wa wajumbe wa chama cha Wananchi nchini Pakistan

Sherry Rehman, mmoja wa wajumbe wa chama cha Wananchi nchini Pakistan amejibu matamshi ya Trump kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, Marekani inafanya njama ya kujaribu kuonyesha kuwa Pakistan ni nchi isiyofaa kuaminika. Naye Shireen Mazari, mwakilishi na kiongozi wa ngazi ya juu wa chama cha 'Tahrik Insaf' kinachoongozwa na Imran Khan sambamba na kuyataja matamshi hayo ya Trump kuwa yasiyo ya haya amesema kwamba, Pakistan imepoteza askari na raia wake wengi katika vita ambavyo haikutakiwa kushirikiana na Marekani. Aidha Marazi ameitaka serikali ya Islamabad kuzuia huduma zote za mawasiliano ya anga na ardhi na Marekani. Hii ni mara ya pili kwa Rais Donald Trump kutoa matamshi makali na ya dharau dhidi ya Pakistan tangu alipoingia White House mwezi Januari mwaka jana.

David Hale, balozi wa Marekani nchini Pakistan

Mwezi Agosti mwaka jana pia katika kutangaza stratijia mpya za nchi yake katika vita dhidi ya Afghanistan, Trump aliituhumu Pakistan kwamba inaunga mkono magaidi sambamba na kuwapatia hifadhi makundi yenye siasa kali, matamshi ambayo pia yalijibiwa kwa maneno makali kutoka kwa Islamabad. Kwa mtazamo wa Trump, dola bilioni 33 za msaada wa kifedha ambazo zimekuwa zikitolewa kwa Pakistan tangu mwaka 2001 hadi sasa ni hatua ya kipumbafu na kwamba katika mwenendo huo, Washington haikunufaika vyovyote vile na msaada wa Islamabad hasa katika mapambano dhidi ya ugaidi kama ambavyo pia pesa hizo hazikusaidia hata kidogo katika vita dhidi ya kundi la Taleban nchini Afghanistan. Stratijia za Trump kuilenga Pakistan zinazojumuisha vitisho vya kukata ushirikiano na misaada ya kifedha na kijeshi kwa Islamabad, zinaweza kuwa na matokeo hasi yanayoweza kuidhuru Marekani yenyewe.

Sheikh Rasheed Ahmad, mkuu wa chama cha 'Muslim League' aliyemkosoa pia Trump

Kuhusiana na suala hilo, Vahid Mojdeh mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Afghanistan "Sambamba na kuashiria stratijia mpya za Marekani kuhusiana na nchi hiyo, amesema kuwa, mashinikizo ya Washington dhidi ya Pakistan yatapelekea kuongezeka vita na kushtadi machafuko nchini Afghanistan." Mashinikizo ya Marekani dhidi ya Pakistan yanatokana na msimamo wa Washington uliojengeka juu ya lugha ya vitisho na dharau dhidi ya nchi nyingine na bila shaka jambo hilo litakabiliwa na hasira kali za serikali, wananchi na hata makundi ya kisiasa na kidini ndani ya taifa hilo. Kitendo cha kutokubaliwa ombi la Waziri Mkuu wa Pakistan la kukutana na Rais Donald Trump kando ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mwezi Septemba mwaka jana, kilitafsiriwa na duru za kisiasa na vyombo vya habari nchini Pakistan kuwa ni dharau ya White House kwa Islamabad.

Shahid Khaqan Abbasi, Waziri Mkuu wa Pakistan

Aidha kadiri mashinikizo ya Marekani dhidi ya Pakistan yanavyozidi kuongezeka, ndivyo ukaribu na ushirikiano wa Islamabad na China na Russia unavyozidi kuimariska, nchi ambazo ni washindani wakubwa wa Marekani katika uga wa kimataifa. Kuhusiana na suala hilo, Ahmad Saidi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Lengo la Pakistan ni kuionyesha Marekani kwamba ikiwa hauna haja na sisi, basi na sisi tutalazimika kuwa marafiki wa China na Russia." Mwisho wa kunukuu. Ndio maana Marekani kutokana na wasi wasi wake wa kuimarika ushirikiano wa Pakistan, China na Russia ikakimbilia lugha ya vitisho, tuhuma na kutishia kuikatia Islamabad misaada ya kifedha.

Tags

Jan 03, 2018 13:16 UTC
Maoni