• Erdoğan: Tutakabiliana na Marekani baada ya kukataa kumrejesha Gülen

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametishia kwamba, ikiwa Marekani itaendelea kukataa ombi la Ankara la kumrejesha nyumbani Fethullah Gülen ambaye anatafutwa na Uturuki, basi nchi hiyo nayo italazimika kuchukua hatua za kukabiliana na Washington.

Erdoğan amesema kuwa, hadi sasa Ankara imeshaikabidhi Washington washukiwa 12 wa ugaidi kwa mujibu wa ombi la Marekani, lakini Washington imekataa kumkabidhi Fethullah Gülen anayetuhumiwa kuratibu mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli tarehe 15 Julai 2016 nchini Uturuki. Ameongeza kwamba, siasa hizo zinazokinzana za viongozi wa Marekani zitapata jibu kutoka kwa Ankara.

Rais wa Uturiki Recep Tayyip Erdoğan akiwa na Donald Trump

Kwa upande wake, Mevlüt Çavuşoğlu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Jumatano iliyopita alitangaza kwamba, mahusiano ya Ankara na Washington yameingia doa kufuatia hatua ya Marekani kukataa kumrejesha Muhammed Fethullah Gülen, kiongozi wa harakati ya Kiislamu na kadhalika hatua ya Marekani kuwaunga mkono waasi wa Kikurdi nchini Syria.

Serikali ya Ankara kwa mara kadhaa imekuwa ikiitaka Washington kumkabidhi shakhsia huyo lakini viongozi wa Marekani wametangaza kuwa mahakama za Marekani zinahitaji kupewa ushahidi wa kutosha unaothibitisha tuhuma za Gülen.

Tags

Jan 12, 2018 04:33 UTC
Maoni