• Rais Putin: Kiongozi wa Korea Kaskazini ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa akili

Rais Vladmir Putin wa Russia amesema kuwa, Kim Jong-un Kiongozi wa Korea Kaskazini, ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa akili na aliyepikika.

Rais Putin aliyasema hayo jana Alkhamisi alipozungumza na vyombo vya habari nchini kwake na kuongeza kwamba, kiongozi wa Korea Kaskazini ni mshindi wa mgogoro ulioibuliwa kati ya nchi yake na Marekani pamoja na waitifake wake.

Mgogoro katika eneo la Peninsula ya Korea, ulishtadi kufuatia siasa za kupenda kujitanua za Rais Donald Trump wa Marekani.

Rais Vladmir Putin wa Russia

Washington inaitaka serikali ya Pyongyang kusimamisha majaribio yake ya kijeshi na silaha za nyuklia; hata hivyo Korea Kaskazini imekuwa ikisisitiza kwamba, maadamu Marekani na marafiki wake wanaendeleza vitisho dhidi yake, nchi hiyo pia itaendelea kujiimarisha kijeshi na kupanua uwezo wake wa kujilinda. Kadhalika Rais Vladmir Putin ameelezea mgogoro ulioibuliwa kati ya Moscow na Washington kuhusiana na masuala ya uchaguzi nchini Marekani mwaka 2016 na kusema, ni Washington ndio inatakiwa kuboresha mahusiano ya nchi mbili na sio nchi yake.

Rais Putin na Trump

Amefafanua kwa kusema kuwa, madai yanayotolewa na viongozi wa Marekani juu ya uingiliaji wa Russia katika uchaguzi wa Marekani ni ya kipuuzi na hayana maana. Amesema, Marekani inapaswa kuelewa kwamba madai hayo hayana faida yoyote ghairi ya kuisababishia hasara nchi hiyo yenyewe. Kadhalika Moscow imekuwa ikikanusha madai hayo ya Marekani na kusisitiza kuwa, haikuingilia uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.

Tags

Jan 12, 2018 04:37 UTC
Maoni