• Korea Kaskazini yatabiri kwamba Trump ataporomoka kisiasa mapema sana

Serikali ya Korea Kaskazini kupitia gazeti la chama tawala nchini humo limemtabiria Rais Donald Trump wa Marekani kuporomoka kisiasa baada ya kuchapishwa kitabu cha 'Moto na Ghadhabu Ndani ya White House ya Trump' kilichoandikwa na Michael Wolff.

Gazeti la Rodong Sinmun ambalo ni la chama tawala nchini Korea Kaskazini limeandika kwamba: Kuuzwa kitabu hicho si tu kumeamsha haraka hisia za upinzani dhidi ya Trump, bali kimeakisi pia uhalisia wa rais huyo kwa jamii ya kimataifa ambapo sasa kiongozi huyo wa Marekani amejikuta akifanyiwa maskhara duniani kote.

Kiongozi wa Korea Kaskazini akimcheka Trump

Katika makala hayo, Rodong Sinmun limeelezea radiamali ya Trump na sababu ya kuuzwa sana kwa kitabu hicho ndani na nje ya Marekani. Kitabu hicho kimeandikwa kwa kutegemea mahojiano aliyoyafanya Michael Wolff na viongozi wa ngazi ya juu wa serikali akiwemo Trump mwenywe. Uchapishwaji wa kitabu hicho umeibua hasira ya Trump kiasi cha kuwafanya mawakili wa rais huyo kuibua makelele wakitaka kusimamishwa mauzo yake.

Trump aliyekasirishwa na kitabu hicho

Katika kitabu hicho ambacho kimeorodhesha matukio ya ndani ya White House katika mwaka wa kwanza wa uongozi wa rais huyo, mwandishi alifanya mahojiano na watu wa karibu na Trump akiwemo pia mshauri wa zamani wa rais huyo, Stephen K. Bannon. Aidha katika kitabu hicho kumeelezwa kuwa hivi sasa White House inatawaliwa na ghasia na mizozo ya kila mara inayosababishwa na uhaini na kulipiza visasi.

Tags

Jan 12, 2018 07:56 UTC
Maoni