Jan 12, 2018 13:19 UTC
  • Kufutiliwa mbali safari ya Trump mjini London

Rais Donald Trump wa Marekani ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba amefutilia mbali safari yake ya nchini Uingereza.

Amesema sababu ya kufutilia mbali safari hiyo inatokana na upinzani wake wa sehemu lilikojengwa jengo jipya la ubalozi wa nchi hiyo mjini London na vilevile gharama zake kubwa. Pamoja na hayo inaonekana kuwa kutoridhishwa na mipango ya mapokezi yake pamoja na wasiwasi wa Waingereza kufanya maandamano dhidi ya  Marekani wakati wa kufanyika safari ya Trump mjini London ni sababu muhimu iliyopelekea kufutiliwa mbali safari hiyo. Kabla ya hapo Trump alikuwa ametaka safari yake mjini London ichukuliwe kuwa ni safari rasmi ambapo alitakiwa kukutana na Malkia Elizabeth wa Uingereza, lakini inaonekana Waizri Mkuu Theresa May alipinga jambo hilo na kuzusha hadhi ya safari hiyo kuwa ya kiwango cha safari ya kikazi tu, na wakati huohuo kufutilia mbali uwezekano wa Trump kukutana na malkia wa Uingereza, jambo ambalo halikumfurahisha Trump.

Rais Trump wa Marekani

Ni wazi kuwa sababu za kufutiliwa mbali au kuakhirishwa safari ya Tump mjini London ni zaidi ya suala la kukutana na Malkia Elizabeth. Licha ya kuwa kuna 'uhusiano maalum' kati ya Uingereza na Marekani na daima Washington na London zimekuwa zikisema zina uhusiano wa karibu zaidi wa kisiasa na kijeshi kuliko nchi nyingine zote, lakini katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na mvutano mkubwa kati ya nchi mbili hizo tokea Trump aingie madarakani nchini Marekani. Jumbe za mara kwa mara za mtandao wa kijamii wa Twitter za Trump katika kukosoa mipango ya Uingereza ya kupambana na ugaidi na vilevile za uungaji mkono wa rais huyo wa Marekani kwa mirengo ya kulia na yenye misimamo mikali ya Uingereza zimewakasirisha sana  viongozi wa nchi hiyo ya Ulaya. Wakati huohuo serikali ya Trump imekasirishwa na misimamo ya Uingereza kukosoa na kulaani uamuazi wa serikali ya Marekani wa kujiondoa katika mkataba wa kimataifa wa mazingira wa Paris na vilevile uamuzi wa hivi karibuni wa Trump kuitambua Beitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala ghasibu wa Israel.

Bi Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza

Kwa matazamo wa viongozi wa Marekani, kuchukuliwa misimamo kama hiyo na viongozi wa Uingereza ni aina fulani ya dharau kwa rais wa Marekani. Hii ni katika hali ambayo Waingereza wamesema mara kadhaa kwamba siasa za kimaslahi za Wamarekani zinazotekelezwa kupitia nara kama vile za 'Marekani Kwanza' zimefanya uungaji mkono wa viongozi wa Uingereza kwa Marekani kuwa mgumu. Ugumu huo umekuwa ni tatizo kubwa hata kwa wahafidhina wa Uingereza ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiunga mkono uhusiano wa pande mbili wa Bahari ya Atlantic na Washington, kwa kadiri kwamba katika hatua isiyo ya kawaida, wahafidhina hao wa Uingereza wameituhumu serikali ya Marekani kuwa inaingilia kati masuala ya ndani ya Uingereza kwa kuyaunga mkono makundi ya mrengo wa kulia ambayo yanatuhumiwa na serikali ya London kuwa yanajihusisha na vitendo vya ugaidi.

Jeremy Corbyn, Mkuu wa Chama cha Leba nchini Uingereza

Hii ni katika hali ambayo awali Jeremy Corbyn, mkuu wa chama cha Leba cha Uingereza na Waziri Mkuu Kivuli wa nchi hiyo alikuwa amewataka Waingereza wajitokeze kwa wingi kuandamana katika mitaa ya mji mkuu London wakati wa kufanyika safari ya Trump kwa ajili ya kulalamikia siasa za serikali ya hivi sasa ya Marekani. Kufanyika maandamano hayo dhidi ya rais wa Marekani katika safari yake ya kwanza nchini Uingereza, tena nchi ambazo zina 'uhusiano maalum', ni jambo lililowatia wasiwasi mkubwa viongozi wa Marekani. Kwa msingi huo inaonekana kuwa jengo la thamani ya dola bilioni moja la ubalozi wa Marekani mjini London, ambalo linachukuliwa kuwa jengo ghali zaidi lililowahi kujengwa na serikali kuu ya Marekani, litafunguliwa na Rex Tillerson,Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani badala ya Rais Donald Trump mwenyewe.

Tags

Maoni