• Dunia yaghadhabishwa na maneno machafu ya Trump dhidi ya wahajiri

Asasi za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zimelaani matamshi machafu yaliyojaa chuki, kejeli na dharau yaliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani alipokuwa akiashiria wahajiri kutoka nchi kadhaa duniani hususan za Afrika wanaoenda kutafuta hifadhi Marekani.

Rupert Colville, msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amewaambia wanahabari mjini Geneva kuwa, maneno yaliyotolewa na rais wa Marekani dhidi ya wahajiri hayana tafsiri nyingine ghairi ya 'maneno ya kibaguzi na machafu' yaliyotolewa kwa lengo la kuhamasisha chuki dhidi ya kundi fulani la watu, na matokeo yake ni kusambaratishwa kwa maisha ya watu wengi.

Naye William Spindler, Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amesema wahajiri wanaokimbia nchi zao, wana haki ya kulindwa na kuheshimiwa katika nchi yoyote ile wanakoenda, pasina kujali rangi, dini, kabila na nchi wanazotokea.

Jana Alkhamisi katika mkutano na maseneta kuhusu kadhia ya uhajiri, na huku akiashiria raia wa Afrika, Haiti na el-Savador, Trump kwa kejeli na dharau alihoji,  "Kwa nini watu wote kutoka nchi chafu wanaendelea kuja katika nchi hii? "

Maandamano ya hivi karibuhi dhidi ya Trump nje ya jengo lake mjini New York

Msemaji wa Umoja wa Afrika, Ebba Kalondo sambamba na kulaani kauli hiyo ya Trump, amesema umoja huo umeshtushwa na matamshi hayo ya kibaguzi; huku baadhi ya nchi za Afrika kama vile Botswana, zikiwaita mabalozi wa Marekani katika nchi hizo kulalamikia matamshi hayo ya chuki ya Trump.

Kwa upande wake Linda Dorcena Forry, Seneta wa chama cha Democrats nchini Marekani ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: "Ni jambo la kusikitisha namna kila mara tunatoa taarifa za kulaani matamshi ya chuki yanayotolewa na eti rais wetu. Ni jambo la kufedhehesha namna sisi wenyewe Wamarekani, tuliamua kumchagua mtu mpumbavu, asiye na haiba na ambaye amejawa na chuki za kibaguzi katika ofisi kubwa zaidi duniani." 

Trump ameshambuliwa vikali na watumiaji wa mitandao ya kijamii kote dunia pamoja na Maseneta na wanasiasa wengine kutoka vyama vya Republican na Democrats nchini Marekani, kutokana na matamshi hayo.

 

Tags

Jan 12, 2018 14:02 UTC
Maoni