• Matusi ya Trump dhidi ya Waafrika yazidi kulaaniwa

Mabalozi wa nchi 54 za Afrika katika Umoja wa Mataifa wamelaani vikali matusi na kejeli za rais wa Marekani dhidi ya Waafrika.

Jana Ijumaa, mabalozi wa nchi 54 za Afrika katika Umoja wa Mataifa walitoa tamko la pamoja na kulaani matusi na matamshi ya kibaguzi na ya kudhalilisha ya rais wa Marekani, Donald Trump aliyoyatoa dhidi ya nchi za Afrika na Wamarekani wenye asili ya Afrika na kumtaka aombe radhi rasmi na afute matusi yake.

Polisi wakikandamiza mtu mweusi nchini Marekani

 

Mabalozi hao wameelezea kusikitishwa kwao na kuendelea ubaguzi wa serikali ya Marekani na hususan Donald Trump dhidi ya wahajiri wa Afrika na wa Amerika ya Latini.

Juzi Alkhamisi, Trump alitoa matusi makali sana dhidi ya Waafrika na nchi za Amerika ya Latini za Haiti na El Salvador na kuitaka Marekani iache kupokea wahajiri kutoka maeneo hayo.

Haiti imekasirishwa mno na kejeli hizo za Trump na kumwita balozi wa Marekani nchini humo ili kumkabidhi rasmi malalamiko yake.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na haki za binadam nayo jana ilitoa taarifa na kuyaita matusi hayo ya Trump kuwa ni ubaguzi wa wazi wa rangi.

Botswana na Senegal zimewaita mabalozi wa Marekani kulalamikia kejeli hizo za Trump huku balozi wa Marekani nchini Panama, John Feeley, akijiuzulu na kusema hawezi kufanya kazi chini ya serikali ya mtu asiyejiheshimu kama Donald Trump.  

Tags

Jan 13, 2018 07:49 UTC
Maoni