• Russia: Habari kwamba tunataka kufungua kambi za kijeshi Libya na Misri ni uongo

Mkuu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Baraza la Shirikisho la Russia amesema kuwa, serikali ya Moscow, haina nia yoyote ya kuanzisha kambi za kijeshi katika nchi za Misri na Libya.

Viktor Bondarev ameyasema hayo baada ya kuenea uvumi kwamba Russia inataka kuanzisha kambi za kijeshi nchini Misri na Libya na kusisitiza kuwa, kwa sasa Moscow haina mpango wowote wa kuanzisha kambi za kijeshi katika nchi hizo. Ameongeza kwa kusema kuwa, suala la Russia kuanzisha kambi na vituo vya kijeshi nje ya nchi ni la mantiki na lenye mpangilio na maandalizi maalumu. 

Viktor Bondarev, Mkuu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Baraza la Shirikisho la Russia

Viktor Bondarev amesisitiza kwamba, Moscow haina nia ya kutaka kujitanua duniani, bali inataka kuwepo mfumo wa dunia nzima wenye kambi kadhaa kwa maslahi ya nchi zote.

Katika uwanja huo Alain Rodier, mtaalamu wa kituo cha utafiti wa usalama nchini Ufaransa hivi karibuni aliliambia gazeti la Atlantico kwamba, hivi sasa Russia mbali na kuwa na kambi za kijeshi mji wa Tartus na Hmeimim nchini Syria, inakusudia pia kuanzisha kambi zingine kama hizo nchini Misri na Libya. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa nchi hiyo hadi sasa bado hawajatoa maelezo yoyote kuhusiana na habari hiyo.

Tags

Jan 13, 2018 14:02 UTC
Maoni