Jan 26, 2018 03:59 UTC

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amesema mbele ya Baraza la Kimataifa la Uchumi mjini Davos Uswisi kwamba nchi za Ulaya zinapaswa kubadilisha siasa zao za kuitegemea Marekani katika masuala ya ndani na nje ya bara hilo.

Kansela huyo wa Ujerumani amesisitiza kwamba, ushirikiano baina ya nchi za dunia ni jambo la lazima, lakini si sahihi kutegemea wengine hata katika masuala ya ndani. Kwa upande wake Christoph Leitl, mkuu wa ofisi za biashara za nchi za Ulaya zinazojulikana kwa jina la 

 

ametilia mkazo maneno hayo ya Merkel na kuilamumu Marekani kwa kujikumbizia kila kitu upande wake na kuzilazimisha nchi nyingine ziifuate kila inachosema hata katika masuala ya vikwazo vyake dhidi ya nchi nyingine. Amesema, nchi za Ulaya zina wajibu wa kujipapatua kutoka katika makucha ya Marekani.

Matamshi ya viongozi hao wawili wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi wa barani Ulaya kuhusiana na siasa za kibeberu za Marekani katika masuala ya ndani na nje ya nchi za Ulaya ni uthibitisho wa kuzidi kuwa mkubwa mpasuko baina ya pande mbili za Bahari ya Atlasi. Mtafiti wa Kifaransa, Marie-Cécile Naves amesema, lengo la siasa za Marekani ni kutaka kuondoa dunia ya kambi kadhaa na kuifanya Marekani bali Trump mwenyewe kuwa mtu mwenye sauti ya mwisho duniani. 

Ukweli wa mambo ni kwamba, msimamo wa Kansela wa Ujerumani unatofautiana kikamilifu na ule wa rais wa Marekani, Donald Trump. Trump anaamini kuwa siasa za kibeberu na za kutumia mabavu za Marekani zitaongeza nguvu za nchi hiyo na kuiwezesha kuwashinda wapinzani wake wote msimamo ambao unakinzana kikamilifu na ule wa Angela Merkel. Huko nyuma Marekani na nchi za Ulaya zilikuwa zinaonekana zina lengo na msimamo mmoja katika masuala ya kimataifa. Hata hivyo tangu Trump alipoingia madarakani nchini Marekani mwezi Januari 2017 na kuja na siasa za "Marekani Kwanza," misimamo mingi ya Marekani imekuwa inakwenda kinyume na manufaa ya nchi za Ulaya. Tangu wakati huo tumekuwa tukiwaona viongozi wa nchi za Ulaya wakikosoa, kulalamikia na kupinga waziwazi misimamo na siasa mpya za Marekani na hususan za Trump. Ni jambo lisilofichika tena kwamba hivi sasa kuna mzozo mkubwa baina ya Marekani na nchi za Bara Ulaya. Misimamo ya Donald Trump inayokinzana na ya Umoja wa Ulaya inashuhudiwa waziwazi katika masuala muhimu, iwe ni yale yanayohusiana na uhusiano wa pande mbili, au ya kimataifa. Hata viongozi wa nchi kama Uingereza ambayo ni muitifaki wa  jadi na wa karibu zaidi wa Marekani barani Ulaya wamekuwa wakilalamikia vitendo vya Donald Trump. Mbali na kulalamikiwa na nchi kama Ujerumaini na Ufaransa, hali imekuwa mbaya hivi sasa kiasi kwamba hata muundo wa uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Marekani nao umebadilika kutoka ushirikiano wa kiistratijia na kubakia ushirikiano tu usio na 'kichombezo' cha kiistratijia.

 

Moja ya sehemu zilizo na mgogoro mkubwa baina ya Marekani na Bara Ulaya ni Maafikiano ya Hali ya Hewa ya Paris. Maafikiano hayo yamethibitisha kuwa misimamo ya Ulaya na Marekani ni tofauti kabisa katika baadhi ya msuala muhimu. Ndio maana mwito wa kuzitaka nchi za Ulaya ziwe huru na zijipapatue kutoka katika makucha ya Marekani kwenye masuala muhimu ya biashara, usalama na hali ya hewa, ukaongezeka sana hivi sasa. Msimamo wa Umoja wa Ulaya unatofautiana pia katika suala la maafikiano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 maarufu kwa jina la maafikiano ya JCPOA. Baada ya maafikiano hayo, nchi za Ulaya zimewekeana mikataba mbalimbali ya pande mbili na Iran, sasa Marekani inadharau manufaa yote hayo ya nchi za Ulaya na kuzusha chokochoko hizi na zile kwa sabaha ya kuyavuruga maafikiano ya JCPOA. Christoph Leitl, mkuu wa ofisi za biashara za nchi za Ulaya anasema, kutokana na vikwazo vinavyowekwa na Marekani dhidi ya nchi nyingine kama Iran na Russia, nchi za Ulaya zinapoteza manufaa yake kwa faida ya upande mmoja ya Marekani. 

Kwa kweli matamshi ya kiongozi kama huyo wa Ulaya na viongozi wengine wakuu wa Umoja wa Ulaya kama wa Ufaransa na Kansela wa Ujerumani ni uthibitisho usiokanushika kuwa mivutano baina ya Ulaya na Marekani inazidi kuwa mikubwa na tutarajie kuongezeka mivutano hiyo katika kipindi cha urais wa  mtu kama Donald Trump huko Marekani.

Christoph Leitl

 

Tags

Maoni