Feb 08, 2018 11:04 UTC
  • Kuelekezewa kidole cha shutuma Marekani za kuwasha moto wa vita Afghanistan

Hamid Karzai, rais wa zamani wa Afghanistan ameishutumu Marekani kuwa inakoleza moto wa vita ndani ya nchi hiyo kwa ajili ya manufaa na maslahi yake.

Kwa mujibu wa Hamid Karzai, amani na usalama umevurugika zaidi nchini Afghanistan baada ya nchi hiyo kushambuliwa na kuvamiwa kijeshi na Marekani mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Rais wa zamani wa Afghanistan amesema, ana wasiwasi kutokana na hali ya usalama nchini humo kuzidi kuwa mbaya na ameitaka serikali kufanya jitihada za kudhamini usalama na kurejesha amani ndani ya nchi.

Aliyekuwa rais wa Afghanistan, Hamid Karzai

Karzai anaitakidi kuwa, kulidhibiti eneo ndio lengo la Marekani la kuongeza idadi ya vituo vyake vya kijeshi nchini Afghanistan. Hii si mara ya kwanza kwa rais wa zamani wa Afghanistan kuitaja Marekani kuwa ndiye msababishaji na mhusika mkuu wa kuendelea kuvurugika usalama na kukosekana amani ndani ya nchi yake. Katika kipindi cha miaka 16 iliyopita, Marekani imekuwa ikifuatilia malengo kadhaa nchini Afghanistan kupitia mkakati wake wa kukaza na kulegeza kamba za udhibiti wa mgogoro na machafuko yanayoendelea nchini humo. Lengo la kwanza la Washington ni kupata kisingizio cha kuhalalisha kuendelea kuwepo kwake kijeshi katika ardhi ya nchi hiyo. Pili ni kuwa, katika anga hiyo ya machafuko na mivutano, Marekani na waitifaki wake ikiwemo Uingereza wanaendelea kupora  maliasili za madini ya Afghanistan. Na tatu ni kwamba kwa kuendelea machafuko na mgogoro nchini Afghanistan, mbali na Washington kufanya kila njia ili kuhakikisha wimbi la machafuko na mapigano linaenea nchi nzima, imekusudia pia kuusambaza ugaidi katika nchi za Asia ya Kati hadi kwenye mipaka ya China. Kutochukua hatua za dhati Marekani za kupambana na kundi la Taliban na kuweza kundi la kigaidi na kitakfiri la DAESH kupiga kambi ndani ya ardhi ya Afghanistan kunadhihirisha malengo ya muda mrefu iliyonayo Washington katika nchi hiyo na eneo zima kwa jumla. Kwa niaba ya Marekani, makundi hayo yanaendelea kuvuruga amani na kuchafua anga ya usalama wa Afghanistan na eneo zima ili Washington iweze kuzihadaa fikra za waliowengi na kutekeleza mipango yake ya kiusalama na kiuchumi iliyokusudia ndani ya nchi hiyo na katika eneo pia.

Magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh nchini Afghanistan 

Saeedi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Afghanistan anasema:

"Wamarekani na Wamagharibi wengine hawakumiminika Afghanistan kwa ajili ya kuikarabati na kuijenga nchi hii, isipokuwa kila mmoja ana malengo yake maalumu na ya kistratijia anayoyafuatilia. Wanachofikiria ni kupata manufaa yao nchini Afghanistan na katika eneo."

Baada ya Marekani kuivamia na kuikalia ardhi ya Afghanistan, mbali na kuyapatia mashirika ya Magharibi zabuni za kuikarabati nchi hiyo iliyaingiza pia nchini humo mashirika ya binafsi likiwemo la Black Water kwa kisingizio cha kusimamia usalama wa vituo vya kiuchumi na kidiplomasia vya nchi za Magharibi. Kwa mujibu wa Hamid Karzai, mashirika hayo ya binafsi yamehusika na uharamia na utekaji nyara watu, mbali na kutenga jela mahususi za kufanyia jinai zisizohesabika dhidi ya wananchi wa Afghanistan.

Ukweli huo ameukiri hata naibu wa balozi wa zamani wa Marekani mjini Kabul David Sandy ambaye amesema:

"Mienendo isiyofaa iliyoshuhudiwa katika mashirika ya usalama ya binafsi yameharibu fikra za watu kuhusiana na mashirika hayo. Baadhi ya watu wanaofanya kazi katika mashirika hayo walikuwa wakiendesha magari wakiwa wamelewa na kuanza kufyatua risasi".

Walinzi wa shirika la Blackwater la Marekani waliotenda anuai za jinai dhidi ya raia wa Afghanistan

Alaa kulli hal, msimamo aliochukua Karzai wakati alipokuwa Rais wa Afghanistan wa kukataa kusaini mkataba wa usalama na Marekani ulionyesha jinsi alivyokuwa na uelewa kamili wa mipango na malengo ya Marekani dhidi ya nchi yake; kwa sababu hata kwa kusiani mkataba huo, Marekani haijachukuia hatua yoyote ya kusaidia kudhamini amani na usalama kwa ajili ya Waafghani. Ukweli ni kwamba mkataba huo wa usalama umetumiwa kama kisingizio tu na Washington ili mbali na kuhalalisha uwepo wa vituo vyake vya kijeshi, ivieneze vituo hivyo katika pembe ya nchi hiyo.../

Tags

Maoni