Feb 08, 2018 14:30 UTC
  • Korea Kaskazini: Maafisa wetu walioenda Korea Kusini hawatokutana na viongozi wa US

Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini imesema kuwa, viongozi wa nchi hiyo waliofanya safari nchini Korea Kusini kwa ajili ya kushiriki katika michuano ya Olimpiki ya msimu wa baridi, kamwe hawatokutana na viongozi wa Marekani.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo mapema leo imesema kuwa, maafisa wa ngazi ya juu waliotuma na serikali ya Pyongyang hawatakuwa na ratiba yoyote ya kukutana na viongozi wa Marekani kando ya michuano hiyo. Kadhalika taarifa hiyo imefafanua kuwa, Korea Kaskazini haiko tayari kushuhudia ubeberu wa Marekani kama ambavyo pia haiko tayari kuvumilia njama za Washington katika kutumia michuano hiyo ya Olimpiki ya msimu wa baridi kali Korea Kusini kwa ajili malengo yake ya kisiasa.

Kim Yong-nam aliyesafiri Korea Kusini kwa ajili ya michuano akiwa nyuma ya Kim Jong-Un kiongozi mkuu wa Korea Kaskazini

Korea Kaskazini inailaumu Marekani kutokana na hatua yake ya kutuma zana nyingi za kijeshi, idadi kubwa ya askari wake na kufanya maneva mbalimbali ya kijeshi katika Rasi ya Korea suala ambalo linatajwa na Pyongyang kuwa lililoshadidisha mgogoro katika eneo hilo. Miongoni mwa shakhsia wa ngazi ya juu waliofanya safari nchini Korea Kusini kwa ajili ya kushirikia sherehe za ufunguizi wa michuano hiyo ni Kim Yong-nam, Kiongozi namba mbili wa nchi hiyo.

Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani, ambaye naye amewasili Korea Kusini

Wakati huo huo, Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani na katika safari yake ya kiduru eneo la Asia, Alkhamisi ya leo amewasili nchini Korea Kusini kwa ajili ya kukutana na Rais Moon Jae-in wa nchi hiyo, ambapo kesho atashiriki katika sherehe za ufunguzi wa michuano hiyo ya Olimpiki mjini Pyeongchang. Michezo hiyo itafanyika tarehe 9 hadi 25 za mwezi huu, huku ile ya walemavu ikipangwa kufanyika tarehe 9 hadi 18 mwezi Machi mwaka huu.

Tags

Maoni